Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) leo Ijumaa Juni 28, 2019 limezindua rasmi safari za kutoka Tanzania kwenda Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Ndege ya ATCL aina ya Airbus 220-300 imeondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam Tanzania (JNIA) saa 4:30 asubuhi ikitarajia kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa OR Tambo, Afrika Kusini saa 6:45 mchana.
Akizungumza na waandishi kabla ya ndege hiyo kuondoka leo Ijumaa, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa amesema lengo la kuanzishwa kwa safari hiyo ni kupunguza muda wa safari kwani abiria walikuwa wanaunganisha ndege ili kufika Afrika Kusini.
Kwandikwa amesema safari hii pia itasaidia kuboresha mahusiano ya kidiplomasia baini ya nchi hizi mbili.
"Tupo tayari kuhudumia Watanzania na tutaendelea kufungua safari nyingi duniani," amesema Kwandikwa
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Emmanuel Koroso amesema Afrika Kusini ni maalumu kwa ajili ya biashara na utalii.
Pia Soma
- Kilichojificha nyuma ya nywele bandia
- Watu 250 mbaroni, sita kortini kwa ugaidi Ethiopia
- Watu 36 wafunikwa na kifusi mgodini DRC
"Tunaomba Watanzania watupe ushirikiano na kupenda vya kwetu, tumeanza safari za kwenda Afrika Kusini na baadaye tunakwenda China na India," amesema
Kuhusu nauli, amesema zinauzwa kwa bei punguza ya Dola za Marekani 299 hadi Julai 15, 2019 kisha baada ya hapo bei mpya zitatangazwa.