Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Mpira wa Kikapu

Vijana Queens kuiwakilisha nchi Champions Afrika

Basketball C0eba192fc Vijana Queens kuiwakilisha nchi Champions Afrika

Wed, 21 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Timu ya Vijana Queens itaiwakilisha nchi kwenye mashindano ya mpira wa kikapu ya wanawake ya nchi za Afrika za kanda ya tano (Champions Cup) yatakayofanyika nchini kwa siku sita kuanzia Septemba 26.

Mbali na Vijana Queens, timu za Alexandria ya Misri, Nile Sisters ya Sudan Kusini, Young Sisters ya Burundi, Rwanda Energy Group na APR za Rwanda, Kenya Ports Authority na Equity za Kenya sanjari na Walkite ya Ethiopia zinatarajiwa kushiriki.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Mwenze Kabinda alisema timu mbili zitakazomaliza kwenye nafasi ya juu kwenye mashindano hayo zitafuzu kushiriki mashindano ya Afrika yatakayofanyika baadae nchini Msumbiji.

Katika hatua nyingine, TBF imesema Oktoba 16-22 Ligi ya Taifa (NBL) itaanza ikishirikisha mikoa 16 ambayo ilifanya Ligi zao za mikoa.

Mabingwa wa Ligi hiyo kwa wanaume na wanawake  watashiriki kwenye mashindano yanayoratibiwa na Shirikisho la Afrika (FIBA).

Mikoa itakayoshiriki NBL ni Arusha, Mara, Dodoma, Iringa, Tabora, Mbeya, Morogoro, Tanga, Rukwa, Mwanza, Kigoma, Shinyanga, Manyara, Kilimanjaro, Mtwara na wenyeji Dar es Salaam.

Wakati huo huo, TBF imewateua Henry Mwinuka, Mohammed Mbwana na Ashraf Harun kuwa makocha wa timu ya taifa itakayojiandaa na mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Afrocan) yatakayoanza Novemba 7-15 yakishirikisha nchi 11.

Kwa wanawake, timu itakuwa chini ya Kablola Shomari, Elizabeth Masenyi na Shomari Alimasi, huku TBF ikiendelea na mchakato wa kupata kocha mwingine msaidizi kwa timu ya wanaume kutoka Zanzibar ikishirikiana na wenzao wa visiwani humo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz