Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Mpira wa Kikapu

Pazi yaanza kusaka tiketi Road to BAL

PAZI BAL FF Pazi yaanza kusaka tiketi Road to BAL

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Pazi inatupa karata yake ya kwanza ya kuwania kufuzu fainali za Klabu Bingwa Afrika (BAL) leo Jumanne itakapocheza na timu ya NBA Junior Academy.

Mashindano hayo ambayo ni hatua ya pili ya kufuzu ‘Ellite 16’ baada ya hatua ya kwanza kufanyika jijini Dar es Salaam yanafanyika kwenye Uwanja wa Ellis Park Arena jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Pazi itacheza mechi tatu ili kufuzu fainali hizo zitakazofanyika nchini Senegal hapo baadaye ambapo mechi zote zitachezwa kuanzia saa 10 jioni kwa mujibu wa ratiba.

Baada ya kucheza na NBA Junior Academy, mchezo mwingine itacheza kesho Jumatano dhidi ya Cape Town Tigers na mechi ya mwisho itakuwa keshokutwa Alhamisi itakapokutana na Dynamos ambayo iliwahi kucheza nayo hatua ya awali.

Katika mchezo huo uliochezwa jijini Dar es Salaam, Pazi iliifunga Dynamos pointi 71-62, hivyo itakutana na timu ambayo wachezaji wake hawatakuwa wageni kucheza pamoja.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Johannesburg, Kocha Msaidizi wa Pazi, Mohamed Mbwana alisema kuwa kikosi kilifika salama na jana kilifanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo.

“Kikosi kiko vizuri na kwenye ari ya juu tayari kwa ajili ya mechi yetu ya kwanza na NBA Academy,” ,” alisema Mbwana na kuongeza:

“Tunajua tuna jukumu la kutetea wana Pazi na taifa kwa ujumla, hivyo tutaanza kwa nguvu na kuhakikisha tunatimiza malengo na kuleta heshima kwa nchi yetu. Mashabiki wa Pazi na wana kikapu kwa ujumla haya mashindano ni magumu lakini hayatukatishi tamaa, tunaamini tunaweza.

“Kila mechi kwetu tunaipa umuhimu na tunaziheshimu timu zote. Hata hao Dynamos ukiangalia hawatakuja kama mara ya mwisho kwa sababu pia wameongeza wachezaji ili kuleta chachu, hivyo sisi tumejipanga kucheza kwa nguvu kwa yeyote tutakayekutana naye maana hii ni hatua nyingine na muhimu kushinda ili tufuzu.”

Nahodha wa timu hiyo, Hasheem Thabeet alisema kuwa: “Mashindano ni magumu. Kila timu iliyokuja huku ama kufuzu hatua hii ni nzuri. Pazi tumekuja kama ‘underdog’ maana ni mara ya kwanza kushiriki. Naamini tutafanya vizuri.”

Chanzo: Mwanaspoti