Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MenuMichezo
Mpira wa Kikapu

Curry kinara wa mastaa watakaolipwa kibosi NBA

Steph Curry LeBron James 072723 Tout 4c1a1cf138304f2dac816f3db189c9c7 Curry kinara wa mastaa watakaolipwa kibosi NBA

Sat, 24 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya supastaa LeBron James kuwa na mvuto zaidi kiasi cha timu yake Los Angeles Lakers kutarajiwa kuongoza kwa mechi zake zisizopungua 40 kuonekana kwenye runinga msimu ujao wa ligi ndefu (regular season), haijatosha kumfanya kuvuna mkwanja mrefu kwa mchezaji mmoja mmoja watakaolipwa zaidi katika NBA.

LeBron mwenye rekodi kibao alizoweka, kuelekea msimu ujao atavuna mkwanja wa Dola 48 milioni na chenji kadhaa, ikiwa ni pungufu ya wachezaji 13 watakaovuna kiasi kikubwa zaidi yake msimu ujao. Hawa hapa mastaa watavuna kuanzia Dola 50 milioni msimu ujao.

STEPH CURRY (GOLDEN STATE WARRIORS)

Huyu ndiye kinara kwenye orodha ya mastaa watakaovuna mkwanja mkubwa zaidi msimu ujao unaoanza Oktoba, ambapo ni bingwa mara nne wa taji la NBA. Curry atakunja Dola 55.7 ikiwa ni zaidi ya Dola 7 milioni juu ya LeBron.

Curry amewaacha mbali mastaa wenzake wanaocheza NBA ambapo thamani yake inatokana na ubora mkubwa alionao, lakini zaidi akiwa na muda zaidi wa kucheza kuliko LeBron ambaye anaelekea ukingoni.

KAWHI LEONARD (LOS ANGELES CLIPPERS)

Ni staa wa Los Angeles Clippers licha ya kutokuwa na mwendelezo mzuri wa kucheza ndani ya timu hiyo kutokana na kukabiliwa na majeraha ya mara kwa mara, lakini ameendelea kulipwa kibosi na timu hiyo ikiamini atawapa taji la NBA kama alivyofanya kwa kila timu aliyocheza ambazo ni San Antonio Spurs na Toronto Raptors.

Kawhi msimu ujao atavuna Dola 52.3 milioni ambapo nyota mwenzake Paul George ameamua kusepa akijiunga Philadelphia 7ers.

JOKIC (DENVER NUGGETS) NA EMBIID (PHILADELPHIA SIXERS)

Nikola Jokic ndiye MVP wa ligi ndefu msimu uliopita akichukua tuzo mikononi mwa Joel Embiid ambaye naye aliitwaa msimu mmoja nyuma na akaumia huku utamu zaidi ni kwamba katika mgawo wa mkwanja wamelingana msimu ujao ambao ni Dola 51.4 milioni na kuwafanya walingane kila kitu na wakitoka kuchukua tuzo hiyo kubwa zaidi kwa mchezaji mmoja mmoja.

KEVIN DURANT-SUNS

Jamaa ni kali mwingine wa NBA ambaye ameshabeba mataji akiwa na Golden State Warriors kabla ya kutimkia Brooklyn Nets na sasa yupo Phoenix Suns akilenga kuchukua taji lingine kama mabosi wa timu hiyo wanavyotamani kiasi cha kumsajili na kumlipa mkwanja mkubwa ili kuongeza nguvu ya ushindi.

Durant ataingiza kiasi cha Dola 51 milioni na chenji kadhaa msimu ujao akiwa na kazi ya kuipa taji timu hiyo yenye utatu mkali ndani ya NBA.

BRADLEY BEAL (PHOENIX SUNS)

Mchezaji mwingine anayecheza na Durant katika timu ya Phoenix Suns huku utatu wao ukikamilishwa na Devin Booker ambaye ndiye anafuatia kwa kulipwa mkwanja mrefu akivuta Dola 49 milioni, huku Bradley Beal aliyesajiliwa kutoka Washington Wizards akitarajiwa kuingiza kiasi cha Dola 50.2 milioni.

Wachezaji wengine wanaolipwa chini ya Dola 50 milioni ambao wapo juu ya LeBron James ni Paul George wa Philadelphia 7ers, Karl-Anthony Towns wa Minnesota Timberwolves na Jaylen Brown wa Boston Celtics watakaokunja Dola Milioni 49.2 milioni, Jimmy Butler Dola 48.8 milioni, Giannis Antetokoumpo na Damian Lillard wanaolingana Dola 48.8 milioni.

Chanzo: Mwanaspoti