Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wimbo ‘Krismas silent night’ watimiza miaka 205

Wimboo Christmass.png Wimbo ‘Krismas silent night’ watimiza miaka 205

Fri, 22 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tuko katika wiki ya kusherehekea sikukuu ya Krismas, ambapo nyimbo nyingi kuhusu sikukuu hiyo zilitungwa zikiwamo zilizokuwa maarufu kwenye baadhi ya maeneo na zilizotamba duniani kote.

Zipo nyimbo maarufu ni lazima zisikike msimu kama huu kila mwaka. Miongoni mwa nyimbo hizo upo unaotimiza miaka 205 mwaka huu, ukiwa umeshaimbwa katika lugha mbalimbali na kutumika kanisani katika ibada.

Wimbo huo unaitwa ‘Silent Night’ ulioimbwa kwa mara ya kwanza katika mkesha wa Krismas mwaka 1818 kwenye Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, kwenye kijiji cha Oberndorf nchini Austria. Padri mmoja kijana aliyeitwa Joseph Mohr, alitunga maneno ya wimbo huo mwaka 1816.

Mwalimu mmoja wa shule ya kijiji cha Arnsdorf, kilichokuwa jirani na Oberndorf, ndiye aliyeweka sauti ya wimbo huu.

Mwalimu huyu Franz Xaver Gruber alikuwa pia anaweza kupiga gitaa na kinanda, alipewa ‘mistari,’ na kuambiwa atunge melodia ya wimbo. Ulipotoka tu ulianza kupendwa sana, na kufikia mwaka 1840 ukawa umeshavuka bahari na kufika Marekani.

Ikumbukwe kuwa zama hizo hakukuwa na redio wala runinga, maonyesho yalikuwa ‘live’, na nyimbo ziliweza kusambaa kwa kutumia nota zilizoandikwa.

Hapa nchini wimbo huo ulianza kuimbwa makanisani, lakini ukajulikana zaidi nje ya makanisa kutokana na toleo lililombwa na marehemu Harry Belafonte na baada ya muda mfupi kuimbwa na Jim Reeves. Wimbo mwingine maarufu katika shamra shamra za Krismasi ni ‘Mary’s Boy Child’wenye hadithi ndefu.

Siku moja mtunzi na mwandishi wa nyimbo Jester Hairston, aliombwa na rafiki yake waliyekuwa wakiishi chumba kimoja, amundike wimbo kwa ajili ya sherehe ya siku ya kuzaliwa ya rafiki yao.

Hairstone akaandika wimbo aliyouita ‘He Pone and Chocolate Tea’, ulikuwa katika staili ya Calypso kwani hafla hiyo ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa rafiki yao ilikuwa inahudhuriwa na marafiki wengi kutoka West Indies, ambako ndiko chanzo cha mtindo wa calypso.

Hata jina la wimbo lilikuwa katika Kiingereza cha watu wa West Indies. Wimbo huo haukurekodiwa, labda kwa sababu ulikuwa ni kwa ajili ya siku hiyo moja tu maalumu.

Baada ya muda Walter Schumann aliyekuwa muongozaji wa kwaya ya Schumann's Hollywood Choir, alimuomba Hairston amtungie wimbo mpya wa Krismas kwa ajili ya kwaya yake. Hairston akauchukua wimbo wake wa ‘He Pone and Chocolate Tea’, akaubadili maneno na kuikabidhi kwaya.

Muimbaji maarufu Harry Belafonte alipousikia wimbo huo ukiimbwa na kwaya akaomba ruksa ya kuurekodi, na mwaka 1956 ukarekodiwa kwa mara ya kwanza.

Mwaka 1957 wimbo huo ukapanda na kuwa wa kwanza katika Top Ten ya Uingereza, na pia kuwa single ya kwanza kuuza nakala milioni moja nchini Uingereza peke yake.

Jim Reeves aliurekodi mwaka 1963 na ndio huo tunaousikiliza kila mwaka. Wanamuziki kama Andy Williams, Bee Gees na John Denver wakaurudia wimbo huu.

Lakini mwaka 1978 Bonney M wakaurekodi tena na kuurudisha upya kwenye Top Ten ya Uingereza na kufikia Novemba 2015 nakala milioni 1.8 za wimbo huo zilikuwa zimeuzwa nchini Uingereza.

Labda pengine ni kwa sababu hii watangazaji wa redio mojawapo walisisitiza mara mbili kuwa wimbo huo umetungwa na Boney M. Nimalizie kwa kutoa historia fupi ya kundi hili la Boney M lililoundwa mwaka 1976 na mtayarishaji wa muziki Frank Farian ambaye ni Mjerumani. Mwaka 1974, Frank Farian alirekodi wimbo ulioitwa ‘Do you wanna dance’ akauandikisha kuwa ulipigwa na kundi lililoitwa Boney M japo wimbo huo ulirekodiwa studio na Frank peke yake.

Baada ya wimbo kupata umaarufu akaamua kutafuta wasanii ili wawe wanaucheza kwenye jukwaa kwa njia ya playback. Na ndipo akawakusanya wasanii wanne Liz Mitchell, Marcia Barret, Maizie Williams na mwanaume pekee Bobby Farell.

Jambo ambalo wengi hawafahamu ni kuwa Frank aliwatumia wanamuziki wawili tu katika kundi lile kurekodi nyimbo za Boney M.

Aliingia studio na Liz Mitchell na Marcia Barrett tu na wawili hawa ndio waliimba nyimbo zote na yeye mwenyewe akawa anaweka sauti nzito ya mwanaume, ambayo jukwaani na kwenye video ilikuwa ikiigizwa na Bobby Farell ambaye kipaji chake haswa kilikuwa ni dansa.

Kundi hili lilikuja kupata umaarufu sana kwani liliweza kuuza zaidi ya santuri milioni 18, nyimbo zao maarufu zikiwemo ‘Daddy Cool’, ‘Ma Baker’ na ule wimbo maarufu wa Krismas ‘Mary’s Boy Child’ Mwaka 1979 ndipo kundi lilipoanza hasa kupata umaarufu mkubwa ulioendelea mpaka kwenye mwaka 1986 ulipoanza kupotea kutokana na mtayarishaji Frank Farian kuanza kujitoa taratibu kuliendeleza kundi hilo.

Baada ya hapo kila mmoja alikuwa akifanya maonyesho yake na wasanii wake lakini wakijitangaza kuwa kundi la Boney M linatumbuiza.

Bobby Farrell, alifariki dunia Desemba 2010.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live