Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watu 94 wafariki dunia baada ya lori la mafuta kulipuka

Lori La Mafuta Libya (600 X 416) Watu 94 wafariki dunia baada ya lori la mafuta kulipuka

Wed, 16 Oct 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Takriban watu 94 wameteketea hadi kufa na wengine 50 wakiwa katika hali mbaya kufuatia moto mkubwa uliosababishwa na mlipuko wa lori la mafuta usiku wa kuamkia jana katika jimbo la Jigawa kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Polisi wa Jigawa waliambia BBC kuwa tukio hilo katika barabara kuu ya Kano-Hadejia lilitokea mwendo wa saa tano na nusu usiku kwa saa za eneo katika kijiji cha Majiya, eneo la serikali ya mtaa wa Taura, ambapo lori lililokuwa limebeba petroli, liliharibika.

Kulingana na msemaji wa polisi, DSP Lawan Shiisu Adam, waathiriwa walikuwa wamekimbilia kuchota mafuta ya petroli iliyokuwa ikivuja kutoka kwa lori lililoharibika wakati cheche iliposababisha mlipuko.

"Wakati mafuta yalipokuwa yakivuja kutoka kwa lori, watu walionywa mara kwa mara kutokaribia mahali hapo.

Polisi walizingira eneo hilo kuzuia watu kwenda eneo la tukio lakini kulikuwa na umati wa watu na waliwazidi nguvu polisi, na kuanza kuchota mafuta yaliyovuja.

Ghafla ukatokea mlipuko,” Bwana Adam alisema.

Wengi wa waathiriwa waliteketezwa kiasi cha kutoweza kutambuliwa.

Wengine ambao walinusurika, walipata majeraha ya viwango tofauti - mengi yakitishia maisha na kukimbizwa hospitalini.

Nigeria inaendelea kushuhudia vifo vya watu wengi vinavyosababishwa na kulipuka kwa malori ya mafuta mara kwa mara.

Mwezi uliopita, takriban watu 48 waliuawa wakati lori la mafuta lilipogongana na gari lingine katika Jimbo la Kati la Niger.

Mamlaka ilisema kuwa lori hilo la mafuta liligongana na lori lililokuwa limebeba wasafiri na ng'ombe, 50 kati yao waliteketezwa wakiwa hai.

Mnamo mwezi Julai 2023, lori la mafuta lililipuka katika jimbo la Ondo Kusini Magharibi mwa Nigeria na kuua watu wasiopungua wanane.

Inasemekana kuwa waathiriwa walikuwa wameenda kuchota mafuta kutoka kwa lori la kubeba petroli ambalo lilihusika katika ajali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live