Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanajeshi 15 wauawa katika mapigano Niger

Wanajeshi Wa Niger Wauawa Katika Shambulio La Kuvizia Wanajeshi 15 wauawa katika mapigano Niger

Wed, 24 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Takriban wanajeshi 15 wa Niger wameuawa wakati wa mapigano na magenge ya kigaidi, magharibi mwa Niger. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya jana Jumanne ya Wizara ya Ulinzi wa Taifa ya nchi hiyo.

Wizara hiyo imeongeza kuwa, tukio hilo ambalo limetokea katika eneo la Bankilare-Tera kwenye mkoa wa Tillabery nchini Niger, pia limepelekea askari 16 kujeruhiwa, wengine watatu kutoweka na magari mawili kuharibiwa.

Taarifa hiyo aidha imesema kuwa, magaidi 21 wameangamizwa katika mapigano hayo hasa baada ya askari wa kuongeza nguvu kufika haraka katika eneo hilo na kumlazimisha adui kukimbia.

Eneo la Tillabery, ambalo liko katika mpaka wa nchi tatu za Niger, Burkina Faso na Mali, linakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya magenge ya kigaidi hasa lile linalojiita tawi la magaidi wa Daesh magharibi mwa Afrika.

Vikosi vya Niger hivi karibuni vimezidisha operesheni za kijeshi katika eneo hilo kufuatia kuongezeka mashambulizi ya magenge ya kigaidi yenye silaha.

Mwezi Machi mwaka huu, Niger, Mali na Burkina Faso chini ya muundo wao mpya Muungano wa Nchi za Sahel (AES) ulitangaza kuundwa kikosi cha pamoja cha kijeshi ili kukabiliana na magenge ya kigaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live