Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stars waifuata Equatorial Guinea

2ac932d5c663ad9e09e14168b6537516 Stars waifuata Equatorial Guinea

Wed, 24 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KIKOSI cha wachezaji 30 cha timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, kimeifuata Equatorial Guinea kwa ajili ya mchezo wa kufuzu fainali za mataifa Afrika, Afcon, unaotarajiwa kuchezwa kesho kutwa nchini humo.

Stars iliyoweka kambi Nairobi, Kenya kwa maandalizi ya mchezo huo ilitarajiwa kuondoka jana jioni baada ya kuwasili wachezaji watatu wanaocheza nje ya Tanzania waliokuwa wamebaki kukamilisha kikosi kinachohitajika.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Clifford Ndimbo alisema wachezaji wanaocheza nje ya Tanzania, Mbwana Samatta, Simon Msuva na Yohana Mkomola watakuwa sehemu ya kikosi hicho.

“Timu itaondokea Kenya na wachezaji wote wako tayari kwa safari hiyo kwenda kupambana kuhakikisha wanapata pointi tatu ugenini ili kutafuta nafasi ya kufuzu. Kocha amesema amefanya maandalizi ya kutosha kushinda mchezo huo,” alisema.

Kikosi kilichotarajiwa kusafiri jana ni Aishi Manula, Metacha Mnata, Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Israel Mwenda, Erasto Nyoni, Bakari Mwamnyeto, Kelvin Yondani, Kenned Juma, Laurent Afred, Mohamed Hussein, Nikson Kibabage, Yassin Mustapha, Simon Msuva na Hassan Dilunga.

Wengine ni Mzamiru Yassin, Jonas Mkude, Feisal Salum, Himid Mao, Salum Abubakari, Farid Mussa, Idd Nado, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, John Bocco, Yohana Mkomola, Shaban Chilunda, Deus Kaseke, Abdul Hamis na Ayoub Lyanga.

Timu hiyo ikiwa imeweka kambi Kenya ilicheza mchezo mmoja ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya huko, Harambee Stars na kufungwa mabao 2-1.

Kocha, Kim Poulsen atakuwa na kibarua cha kwanza cha kutafuta matokeo ugenini katika mchezo huo wa marudiano akichukua mikoba ya Ettiene Ndayiragije aliyefutwa kazi baada ya kufanya vibaya kwenye michuano ya mabingwa wa Afrika, Chan, inayoshirikisha wachezaji wa ndani.

Mchezaji, John Bocco alisema wamefanya maandalizi mazuri kuelekea katika mchezo huo na ana amini watafanya kile walichokikusudia.

Chanzo: www.habarileo.co.tz