Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwamuzi Fifa ataka mechi kumuenzi JPM

264a2bb2de0d48d017d90af51f3c8580.png Mwamuzi Fifa ataka mechi kumuenzi JPM

Fri, 26 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MWAMUZI wa kimataifa wa soka, Florentina Zablon amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kuandaa pambano moja maalumu kwa ajili ya kumuenzi Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili jan, Florentina ambaye ni mwamuzi mwanamke pekee wa Tanzania aliyechezesha mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara huku Rais Magufuli akiwa mgeni rasmi, alisema kiongozi huyo alikuwa mpenda michezo.

Florentina pia alichezesha mchezo wa mzunguko wa 29 kati ya Simba na Kagera Sugar, Uwanja wa Benjamni Mkapa Mei 19, 2018 na Rais Magufuli kuwakabidhi Simba kombe la ubingwa wa ligi msimu wa wa mwaka 2017/18 akisaidiwa na Jese Erasmo, Mashaka Mwandebwa na Hellen Mduma aliyekuwa mezani.

“Nashauri TFF iandae pambano la kumuenzi Rais Magufuli kwa sababu alikuwa anapenda michezo hasa mpira wa miguu na timu ya Tanzania ikifungwa alikuwa anaumia,” alisema.

Florentina pia alisema baada ya kuchaguliwa kuchezesha mchezo huo na kusikia kuwa mgeni rasmi ni Rais Magufuli siku ya mchezo alijitahidi kumuonesha kuwa wanawake wanaweza na ndivyo ilivyokuwa kwani mchezo ulimalizika salama na aliyefungwa alikubali matokeo.

Alisema kifo cha Rais Magufuli kwake kimemuuma ikizingatiwa aliwahi kukutana naye uso kwa uso na kumpongeza kwa kazi nzuri na kuweka saini kwenye mpira ambao anao hadi leo nyumbani kwake.

“Kwanza niliposikia Rais Magufuli amefariki niliona kama ndoto labda nikimaliza kuota itabadilika lakini ni kweli ametutoka, kwangu binafsi nitamkumbuka kwa maneno ya kunifariji aliyoniaeleza baada ya mchezo huo na kusaini mpira ambao ninao hadi leo,” alisema.

Katika mchezo huo aliochezesha Florentina, Simba ilifungwa bao 1-0 na Kagera Sugar na baada ya mchezo huo Rais Magufuli alisema kuwa kwa mpira ambao aliona wakicheza Simba itakuwa ngumu kwao kuleta taji la Afrika katika ardhi ya Tanzania katika kipindi hicho.

Waamuzi wengine waliowahi kuchezesha mechi mbele ya Rais Magufuli ni Martin Saanya ambaye alikuwa mwamuzi wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na Simba, Uwanja wa Mkapa.

Mchezo ambao ulikuwa wa kwanza kwa watani wa jadi Rais John Magufuli kufika uwanjani kushuhudia na Simba kufungwa bao 1-0, Machi 8, 2020.

Wengine ambao waliokuwa wasaidizi katika michezo hiyo ni Mohamed Mkono, Frank Komba na Abdallah Mwinyimkuu, Ramadhan Kayoko walikuwa wasaidizi nyuma ya magoli, huku Hery Sasii akiwa mezani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz