Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtanzania adai kuteswa Iraq alikokwenda kufanya kazi

Boddd.jpeg Mtanzania adai kuteswa Iraq alikokwenda kufanya kazi

Sat, 14 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Upande wa mashtaka katika kesi ya kusafirisha binadamu inayomkabili Mohamed Masoli umedai mlalamikaji (jina limehifadhiwa) baada ya kufika nchini Iraq kwa ajili ya kufanya kazi za ndani aliteswa na bosi wake, ikiwemo kuingiliwa kimwili na wanaume zaidi ya wawili kwa wakati mmoja.

Hayo yalielezwa juzi na Wakili wa Serikali, Mosia Kaima wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Masoli anakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha binadamu kinyume cha sheria.

Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 16, 2021 maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na siku hiyo alimsafirisha mwanamke mmoja jina limehifadhiwa.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ramadhani Rugemalira, Wakili Kaima alidai licha ya shauri hilo kuitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi, mshtakiwa amemuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ya kukiri na kupunguziwa adhabu kwa njia ya makubaliano (plea bargaining).

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Rugemalira aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 25 itakapoendelea kusikilizwa.

Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Wakili Kaima alisoma maelezo ya shahidi ambaye alidai kuwa mlalamikiwa alitoa tangazo la kazi za ndani katika nchi za Kiarabu, ikiwemo Uturuki kupitia mitandao ya kijamii.

Alidai mlalamikaji huyo baada ya kuona tangazo hilo aliwasiliana na mshtakiwa kwa njia ya ujumbe mfupi na alimtajia kazi zinazotakiwa kufanywa ambazo ni kazi za ndani, kuuza duka na kusafisha hospitali.

Kaima alidai mlalamikaji alianza kuandaa hati ya kusafiria na wakapanga kwenda kupima ugonjwa wa Uviko -19 katika Hospitali ya Rufaa ya Amana iliyopo jijini Dar es Salaam.

“Walivyofika Hospitali ya Amana kwa ajili ya kupima Uviko-19 alikutana na wanawake wengine wawili na wenyewe walikuwa wanasafirishwa kwenda nchini Uturuki,” alidai.

Juni 11, 2021 mshtakiwa huyo alimweleza mlalamikaji na wanawake wengine wawili wakutane eneo la Kipawa kituo cha mafuta, ili wakachukue nyaraka za kusafiria na wasaini mkataba wa kazi.

Kaima alidai kwa maelezo ya mlalamikaji anadai baada ya kusaini mkataba huo walipewa nyaraka ya kusafiria, lakini mkataba wa kazi hawakupewa.

Alidai walielekea Uwanja wa Ndege wa Julis Nyerere wakakutana na mtu ambaye hawamjui na aliwapa maelezo wapande ndege ya Dubai na walipofika walishangazwa kuambiwa wapande ndege inayokwenda Iraq, eneo la Kurdistan.

Walipofika Iraq walipokelewa kwenye ofisi na walipokonywa hati zao za kusafiria na wakaingizwa kwenye chumba kimoja na walikuwa wanapewa mlo mmoja kwa siku.

Wakiwa kwenye chumba hicho wanaume wenye asili ya Kiarabu walikuwa wanakwenda kuchagua mwanamke anayemtaka na kuondoka naye.

Kwa mujibu wa maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo, alipata kazi za ndani, lakini bosi wake alikuwa anampiga, anamnyanyasa ikiwemo kupewa chakula mlo mmoja, akiumwa hatibiwi na alikuwa akilazimishwa amsafishe paka.

Pia alikuwa halipwi mshahara na alikuwa anaingiliwa na wanaume zaidi ya wawili kwa wakati mmoja.

Kutokana na hali hiyo, ndipo mlalamikaji akalazimika kuwasiliana na mshtakiwa huyo, ili amrudishe Tanzania kwa kuwa anapata mateso, lakini Masoli alimwambia hawezi kumrudisha hadi arudishe fidia ya Dola 4,000 za Marekani kwenye ofisi yao kwa kuwa amekatisha mkataba.

Baada ya kuelezwa hayo na mshtakiwa, mlalamikaji aliwasiliana na ndugu zake ambao walipeleka malalamiko katika kituo cha Polisi Tabata, Dar es Salaam kwa kushirikiana na Kituo Kikuu cha Polisi walimkamata mshitakiwa na kumlazimisha atumie gharama zake amrudishe ndugu yao nchini.

Baada ya kumrudisha mlalamikaji nchini, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani kwa kosa la kufanya biashara haramu ya binadamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live