Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msuva apania kuimaliza Equatorial Guinea

Msuva Pic Data Msuva apania kuimaliza Equatorial Guinea

Wed, 24 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva anayeichezea Wydad Casablanca ya Morocco, amepania kufanya makubwa kwenye mchezo wa kunia kufuzu kwa Afcon kesho, Alhamisi kwenye uwanja wa Malabo  dhidi Guinea ya Ikweta.

Juni 30, 2020, Shirikisho la soka Afrika lilitangaza  kuwa fainali za Afcon ambazo zilikuwa zikitarajiwa kuwa zitafanyika mwanzoni mwa mwaka huu, zimesogezwa mbele hadi mwakani kuanzia Januari hadi Februari kutokana na janga la virusi vya corona.

Msuva alisema, "Tupo tayari kwa mapambano, naamini Watanzania wapo nyuma yetu hivyo hatutakuwa tayari kuwaangusha, nikiwa kama mchezaji ambaye ni sehemu ya timu nitapambana kwa kutoa mchango wangu wote ili kuhakikisha timu inapata kile ambacho tumekilenga, ushindi yatakuwa matokeo mazuri zaidi kwetu."

Katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi hiyo, Tanzania ambayo ipo kundi  J, inatakiwa kupata  sare au ushindi dhidi ya Guinea ya Ikweta  ili kujiweka pazuri kabla ya kumalizia nyumbani, Tanzania mchezo wa hatua ya makundi dhidi ya Libya.

Taifa Stars ambayo iliweka kambi ya maandalizi nchini Kenya na kucheza mchezo mmoja wa kirafiki ilitua juzi, Guinea ya Ikweta ikiwa na nyota wake 30, akiwemo nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Samatta aliyetokea Uturuki na Msuva ambaye alikuwa Morocco  na Thomas Ulimwengu aliyekuwa DR Congo.

Wakati Msuva na wenzake wakiwa na kazi moja kubwa mbele yao, ukuta wa Taifa Stars unatakiwa kuwa makini ukiongozwa na kipa, Aishi Manula ili kuhakikisha wanawabana vizuri wapinzani wao ambao wanaonekana kuwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa na soka la kimataifa kama ilivyo kwa vijana wa Poulsen.

Guinea ya Ikweta ambao siku chache zilizopita wamemteua Juan Obiang kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa hilo, imekuwa ikiwategemea kiungo,Pedro Obiang na  nyota wengine  watatu kwenye safu yao ya ushambuliaji, Iban Salvador, Josete Miranda na Salomon Obama.

Obiang ni kiungo mwenye asili ya Hispania ambaye aliwahi kucheza soka la kulipwa England akiwa na wagonga nyundo wa London, West Ham United kwa sasa anaichezea  Sassuolo ya Ligi Kuu Italia, Salvador  ambaye  hushambulia akitokea kulia anaichezea CF Fuenlabrada inayoshiriki Ligi daraja la Kwanza Hispania maarufu kama Segunda.

Miranda ambaye ushambulia huku akitokea upande wa kushoto ni mchezaji wa kikosi B cha Getafe CF, Obama anaichezea Sevan FC ya Armenia. Nyota hao ndio wachezaji ambao wamehusika kwa kiasi kikubwa kuifanya Guinea ya Ikweta kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi J wakiwa na pointi  sita. Tanzania ipo nafasi ya tatu na pointi nne.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz