Mganga wa jadi anayefahamika kwa jina la Abdoulaye Kouro anayedaiwa kumlaghai mbunge wa zamani wa Garsen nchini Kenya, Danson Mungatana na kumtapeli pesa kiasi cha Dola za Marekani milioni 1 (sawa na Tsh bilioni 2.322) akidai kwamba angemwekeza katika sekta ya mafuta na kupata faida zaidi.
Kouro alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Milimani ambapo alimuomba kuondoa hati ya kukamatwa kwake iliyotolewa akidai kuwa ni alikuwa mgonjwa na amekuwa akijitibu kwa kutumia dawa za kienyeji kutoka nchini Tanzania.
"Mheshimiwa, nimekuwa mgonjwa. Sikwenda hospitali yoyote, nilichagua kujitibu mwenyewe kwa dawa za mitishamba ambazo ninazitoa Tanzania,” alisema Abdoulaye.
Kuoro ambaye yuko rumande baada ya mahakama kufuta masharti ya dhamana, aliiomba korti imsamehe kwa kushindwa kupata stakabathi za matibabu za kuthibitisha kuwa amekuwa akijitibu.
Mbele ya mahakama hiyo, Mganga huyo alisomewa mashtaka ya kumlaghai mbunge huyo kuwa angezifanya pesa hizo kuongezeka na kupata pesa nyingi zaidi kwa kuwekeza katika biashara ya mafuta.
Kuoro anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Aprili 20 na 29, 2013, katika ghorofa ya Sandalwood, kando ya Barabara ya Brookside huko Westlands, kaunti ya Nairobi, ambapo alikuwa na watuhumiwa wenzake ambao hata hivyo hawajakamtwa.
Kulingana na hati ya mashtaka, mganga huyo anadaiwa kuchukuwa kiasi cha dola 1,000,000 kutoka kwa Danson Mungatana, ambazo ni sawa na KSh 76,000,000 akijifanya kuwa ana uwezo wa kuwekeza kwa niaba yake katika biashara hiyo ya mafuta.
Kouro alishtakiwa pia kwa kukutwa na karatasi za noti bandia huku akijua kuwa ni kosa kisheria. Hakimu Mkuu Wendy Micheni alimweka mtuhumiwa huyo rumande akisubiri kusikilizwa kwa kesi hiyo ambapo Polisi wamewapanga Mungatana na Muteke kama mashahidi.