Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Joash Onyango aangushiwa jumba bovu Kenya

Yanga Onyango Pic Data Joash Onyango aangushiwa jumba bovu Kenya

Sat, 20 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Beki wa kati wa Simba, Joash Onyango anakabiliwa na jukumu zito la kuongoza safu ya ulinzi ya timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars' katika mechi zake mbili za kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Misri na Togo zitakazochezwa baadaye mwezi huu.

Hiyo ni kufuatia kuachwa kwa baadhi ya nyota wenye uzoefu wanaocheza katika nafasi ya beki wa kati katika kikosi cha wachezaji 28 kilichotangazwa leo na kocha mkuu wa timu hiyo, Jacob “Ghost” Mulee.

Kenya inayoshika nafasi ya tatu katika kundi G la mashindano hayo ya kuwania kufuzu ikiwa na pointi tatu, itaanza kwa kuikaribisha Misri nyumbani, Machi 27 na baada ya hapo, Machi 29 itakabiliana na Togo ugenini huko Lome, Machi 29.

Beki wa kimataifa wa Kenya anayecheza Lusaka Dynamos ya Zambia, Musa Mohamed, ameshindwa kujumuishwa katika kikosi hicho cha Harambee Stars kama ilivyo kwa Shakava Haruna wa Gor Mahia na hivyo kumfanya Onyango kuwa mlinzi pekee wa kati mwenye uzoefu mkubwa kikosini kuliko wengine walioitwa.

Kiungo wa CF Montreal ya Canada ambaye pia ndiye nahodha wa Harambee Stars, Victor Wanyama, jina lake halijajumuishwa katika kikosi hicho kama ilivyo kwa winga wa Visel Kobe, Ayoub Timbe 'Masika'.

Hakukuwa na nafasi kwa kipa wa Yanga, Farouk Shikhalo kama ilivyo kwa kiungo wa Simba, Francis Kahata ambao wamekuwa hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara katika vikosi vya timu zao.

Kocha Mulee ameita idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi hiyo akiwemo mshambuliaji tegemeo na aliye moto wa kuotea mbali hivi sasa, Michael Olunga anayeitumikia Al Duhail ya Qatar ingawa pia amewajumuisha baadhi ya wachezaji wa ndani.

Kikosi kamili cha Kenya kinaundwa na makipa Ian Otieno (Zesco United), James Saruni (Ulinzi Stars) na Joseph Okoth (KCB) wakati mabeki ni Joseph Okumu (IF Elfsborg), Eric Ouma (AIK), Joash Onyango (Simba), Johnstone Omurwa (Wazito), Nahashon Alembi (KCB), Harun Mwale (Ulinzi Stars), Daniel Sakari (Kariobangi Sharks) na Baraka Badi (KCB)

Viungo ni Anthony Akumu (Kaizer Chiefs), Duke Abuya (Nkana), Cliff Nyakeya (Masr), Duncan Otieno (Lusaka Warriors), Lawrence Juma (Sofapaka), Kenneth Muguna (Gor Mahia), Kevin Simiyu (Nzoia Sugar), Danson Chetambe (Bandari), James Mazembe (Kariobangi Sharks), David Owino (KCB), Kevin Kimani (Wazito, Kenya), Boniface Muchiri (Tusker) na Abdalla Hassan (Bandari) wakati washambuliaji wakiwa ni Michael Olunga (Al Duhail), Masud Juma (Difaâ Hassani El Jadidi), Erick Kapaito (Kariobangi Sharks) na Elvis Rupia (AFC Leopards)

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz