Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hii hapa mikakati soko la mazao Kenya, DRC, Sudan Kusini

E5a1a39b88ea8d1be30ebb1eaaeb61df Hii hapa mikakati soko la mazao Kenya, DRC, Sudan Kusini

Tue, 5 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Kilimo imesema bidhaa za mazao ya kilimo ukiwamo mtama, mchele na mahindi zitaanza kupelekwa kuuzwa kwenye kituo cha kuuza bidhaa za mazao ya chakula mjini Juba nchini Sudan Kusini.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, alisema juzi kuwa, serikali pia itafungua vituo vya kuuza bidhaa za kilimo na si maghala katika nchi za Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Alisema mchakato wa kufungua kituo hicho mjini Juba umefika mbali na kuna timu ya wataalamu ilikwenda huko kwa mazungumzo na muda si mrefu watatangaza kuanza kufanyakazi kwa kituo hicho ili wafanyabiashara wapate fursa ya kuuza mazao.

Alisema katikati au mwisho wa mwezi huu anatarajia kwenda Juba na wafanyabiashara Watanzania na kwamba mazao yatakayopelekwa ni mtama, mchele na mahindi.

Alivitaja vituo vingine vya kuuzia bidhaa za kilimo kuwa ni Mombasa na Nairobi nchini Kenya, Comoro na zitakazofuata ni DRC na Zimbabwe.

Kuhusu kituo cha Mombasa, Profesa Mkenda alisema kuna mkataba na kampuni inayosaga mahindi zaidi ya tani 100,000 kwa mwaka ili kununua zao hilo kutoka Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), wakati kituo cha Nairobi kipo katika hatua za mwisho ili wakizindue.

Alisema kituo cha Comoro wataalamu wamekwenda ili kuanza kupeleka mchele na baada ya hapo wataelekeza nguvu DRC na Zimbabwe.

Hivi karibuni, Mkurugenzi wa Idara ya Habari -Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema Tanzania ina ziada ya chakula na kwamba serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeanzisha utaratibu wa kuanzisha maghala ya chakula (vituo) kwenye maeneo ambayo bidhaa za Tanzania zinahitajika hasa mazao ya kilimo.

Msigwa alisema vituo hivyo vitafunguliwa katika nchi za Kenya katika mji wa Mombasa, DRC na Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa Msigwa, mwaka huu Tanzania ina ziada ya tani zaidi ya milioni 1.9 za mchele na zaidi ya tani 900,000 za mahindi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema wafanyabiashara wa Tanzania wataruhusiwa kuvitumia vituo hivyo kurahisisha biashara zao.

"Serikali imeanza utaratibu wa kujenga na kukodi maghala katika nchi ambazo zina masoko ya mazao kama vile Sudan Kusini, DRC na Kenya, tunaenda kuweka maghala katika nchi hizo ili Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB) na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) waweke mazao hayo kwenye maghala hayo na kuyauza," alisema Bashe akiwa mkoani Katavi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz