Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ghana kuanzisha kiwanda cha kuunganisha magari Tanzania

Ghana Magari Pic Ghana kuanzisha kiwanda cha kuunganisha magari Tanzania

Fri, 26 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ghana inakusudia kuanzisha kiwanda cha kuunganisha magari nchini Tanzania  ikiwa ni moja ya mipango ya taifa hilo kunufaika na fursa ya Eneo la Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA).

Taifa hilo la Afrika Magharibi lina kiwanda cha kuunda magari, hivyo ujio wa wafanyabiasha wa Ghana kwenye maonyesho ya biashara hapa nchini Tanzania umewaonyesha fursa hiyo kubwa kiuchumi.

Hayo yamebainishwa jana, Januari 25, 2024 na Ofisa Mkuu wa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara ya Ghana, Koffi Oddo aliyemwakilisha waziri wa wizara hiyo, Kobina Hammond katika ufunguzi wa maonyesho ya biashara ya Ghana Expo 2024.

Oddo amesema wataanzisha kiwanda kulingana na mazingira, kwa kuwa wanatambua mazingira ya Afrika yanatofautiana, hivyo watazingatia hilo katika utengenezaji wa magari hayo.

“Tukisharudi Accra, tutakwenda kukaa na watu wa Kantanka (kampuni ya magari) kuwaeleza fursa iliyopo kwao kwenye soko la Tanzania. Watakaa na Wizara ya Uchukuzi kujadiliana namna wanavyoweza kuingia kwenye soko hili,” amesema.

Ofisa huyo amesema lengo la maonyesho hayo ni kutambulisha biashara na bidhaa kutoka Ghana kwenye soko la Tanzania, kuongeza urari wa biashara baina ya mataifa hayo mawili pamoja na kuwaunganisha wafanyabiashara wa mataifa hayo.

“Ushirikiano huu ni ushuhuda tosha wa uimara wa Tanzania kama ulivyo wa Ghana, katika kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika AfCFTA,” amesema ofisa huyo kutoka Ghana.

Kwa upande wake, Meneja katika Usimamizi, Ukuzaji Biashara kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Mohemed Tajiri amesema AfCFTA ni fursa kubwa kwa mataifa ya Afrika katika kukuza biashara.

Amesema kwenye maonyesho ya Ghana Expo2024, wafanyabiashara wamebadilishana mawazo na kujenga muktadha wa kupata bidhaa kutoka Ghana na za Tanzania kuuzwa huko Ghana.

“Tuna matarajio makubwa baada ya maonyesho haya hasa kutokana na nafuu ya kodi inayotolewa kupitia AfCFTA. Pia, wafanyabiashara wataunganishwa moja kwa moja kupitia mkondo huu wa biashara,” amesema.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), Mercy Sila amesema wanawake wako tayari kushiriki kwenye biashara na Ghana na wameanza kunufaika kupitia uhusiano ulioanzishwa baina yao.

“Tunahitaji kujifunza kutoka kwa wenzetu Ghana ili tukuze biashara zetu, ndiyo maana tumeanzisha uhusiano huu ili kubadilisha uzoefu na kukuza biashara zetu,” amesema mwanamke huyo.

Naye Naibu Balozi wa Ghana katika mataifa ya Afrika Mashariki, William Abochi amesema ziara ya wafanyabiashara kutoka Ghana si tu inalenga kutafuta masoko hapa Tanzania, bali pia kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara wa Tanzania.

“Ni muhimu kuwa na ushirikiano ambao utawaweka wafanyabiashara wetu karibu na kuwawezesha kutumia kila fursa iliyo mbele yao katika kukuza biashara na uchumi wa mataifa yetu,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live