Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Covid-19 imepoteza 92% ya mapato utalii EAC’

E8c43a401eb89606ffd69c816cd3f4f6.jpeg ‘Covid-19 imepoteza 92% ya mapato utalii EAC’

Tue, 12 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimepoteza mapato kwa asilimia 92 katika sekta ya utalii kwa sababu ya janga la Covid-19, imebainika.

Katibu Mkuu wa EAC, Dk Peter Mathuki amesema katika kipindi cha janga la Covid-19, watalii waliofika katika ukanda huu walipungua kutoka milioni 6.98 walioingia EAC kabla ya janga hilo hadi milioni 2.25 na kuwa sekta hiyo ndio iliyoathirika zaidi kutokana na janga hilo.

Alisema kwa sasa ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefunguliwa tena kibiashara.

Dk Mathuki alizitaka serikali za nchi washirika wa EAC na wadau wengine kushirikiana kutangaza na kuuza vivutio vya utalii vilivyopo katika ukanda huo sambamba na bidhaa kama sehemu ya juhudi za kurejesha haraka kwa sekta hiyo katika hali bora.

Alikuwa akizungumza katika ufunguzi wa Maonesho ya Kwanza ya Utalii katika nchi wanachama wa EAC kwenye Viwanja vya TGT jijini Arusha, yaliyoanza Oktoba 9 na kutarajiwa kuhitimishwa jana.

“Licha ya ukweli kuwa janga hili limepunguza mapato yaliyokuwa yakipatikana katika sekta ya utalii, tunaamini kuwa kupitia nguvu za pamoja tunaweza kurejea katika mapato tuliyokuwa tukipata kabla ya janga hili na ikiwezekana hata kufanya vema zaidi katika kipindi cha chini ya miaka mitano,” alisema.

Alisema ukanda huo umejifunza mengi kutokana na janga hilo hususan katika uhusiano wa sekta ya uchumi.

Kwa mujibu wa Dk Mathuki, maonesho hayo ya utalii ni moja ya mipango ya kwanza iliyoanzishwa katika kutekeleza Mpango wa Kurejesha Utalii wa Kanda ulioidhinishwa na mawaziri wa Jumuiya ya Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori, Julai 15, 2021.

Alisema EAC pia ilikuwa inapanga kufanya kampeni kubwa ya utalii ya kikanda na ndani katika ukanda huo.

Alisema Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki liliazimia kuwa raia wa EAC wanapaswa kutozwa viwango vya ndani wakati wanaingia katika maeneo ya utalii ya umma kama vile mbuga za taifa na hifadhi zilizopo EAC.

Aliongeza uamuzi huo umetekelezwa na nchi zote washirika na zimeongeza hoteli na vituo vingine vya malazi ya watalii.

Alizitaka nchi washirika wa EAC kubadilisha aina ya utalii kwa kutengeneza bidhaa nyingine kama utalii wa mikutano, utalii wa kitamaduni, utalii wa michezo huku akiipongeza Tanzania kwa kuzindua kampeni ya utalii wa gofu.

Dk Mathuki alisema EAC imeanza shughuli za kuwajengea uwezo watoa huduma mbalimbali wa utalii kama wafanyakazi katika hoteli, waongoza watalii, wakala wa usafiri pamoja na jamii za wenyeji.

“Ujenzi wa uwezo utazingatia mambo muhimu wakati huu kama vile kutekeleza mwongozo wa utalii unaohusiana wa Covid-19. Baada ya kuanza kwa Covid-19, tulifanya mafunzo kwa wafanyakazi walio mstari wa mbele kuhusu hatua za usalama wakati wa janga hili katika viwanja vyote vya ndege vya kimataifa katika nchi washirika wa EAC,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz