Newcastle United inamfuatilia kwa karibu winga wa Bayern Munich na Ujerumani, Leroy Sane, 28, na inataka kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya baridi ambapo mkataba wake utakuwa umebakisha miezi sita kabla ya kumalizika.
Sane ambaye alitajwa kwamba angeondoka Bayern Munich katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, msimu huu hajacheza hata mechi moja kutokana na majeraha yanayomwandama.
Barcelona na timu kadhaa za Ligi Kuu England zilionyesha kuhitaji huduma ya staa huyo katika dirisha lililopita, lakini ilishindikana kumng’oa Alianz Arena. Mkataba wa Sane na Bayern Munich unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na kama akipona majeraha yake kabla ya dirisha lijalo la majira ya baridi mabosi wa timu hiyo wanaweza kufikia uamuzi wa kumuuza ili asiondoke bure mwisho wa msimu. Nyota huyo aliwahi kukipiga Man City kabla ya kurejea Bayen Munich.
Wakati huo huo mabosi wa Bayern Munich wanafanya juhudi kubwa katika kuhakikisha wanamshawishi kiungo Jamal Musiala akubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia kwenye timu hiyo kwa muda mrefu zaidi. Taarifa zinaeleza timu nyingi zimeanza kumuwinda fundi huyo wa kimataifa wa Ujerumani ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2026.
AC Milan, Inter Milan na Napoli zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili kiungo wa Torino na Italia, Samuele Ricci, 23, katika dirisha lijalo la kiangazi. Ricci ambaye ni mmoja kati ya viungo walioonyesha viwango bora msimu uliopita na huu ulioanza, mkataba wake na Torino unatarajiwa kumalizika 2026. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi tano za michuano yote.
LIVERPOOL inataka kwanza mazungumzo na beki raia wa Uholanzi, Virgil van Dijk kwa ajili ya kumuongeza mkataba mpya kabla ya kutuma ofa kwenda Sevilla ili kumsajili beki wa timu hiyo, Mfaransa Loic Bade, 24. Van Dijk ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu hajafikia mwafaka na mabosi wa Liverpool ikiwa atabaki ama ataondoka.
KIUNGO wa Bayern Munich, Joshua Kimmich ambaye anawindwa na timu mbalimbali za England inadaiwa kuwa yupo tayari kusaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia kikosini hapo kwa muda mrefu. Kimmich alikuwa katika rada za Arsenal na Man United zilizotaka kumsajili katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
KABLA ya kujiunga na Rennes akitokea Barcelona, Mikayil Faye alipokea ofa kutoka Manchester United ambayo ilikuwa nono zaidi lakini alikataa kwa sababu anaamini kiwango chake kitakuwa bora zaidi akiwa na wababe hao wa Ufaransa. Faye mwenye umri wa miaka 20, ni miongoni mwa mastaa tegemeo katika kikosi cha timu ya taifa ya Senegal.
BARCELONA bado ina matumaini na mshambuliaji raia wa Hispania, Ansu Fati licha ya kutocheza mechi yoyote tangu Agosti, mwaka huu. Ansu Fati amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara jambo linalosababisha asionekane uwanjani kwa muda mrefu. Msimu uliopita staa huyo alicheza kwa mkopo Bringhton ambako hakuonyesha kiwango bora.
KUNA uwezekano mkubwa mastaa wa West Ham United, Michail Antonio, 34, na Danny Ings, 32, wote wakaondoka dirisha lijalo la majira ya baridi. Wachezaji hao ambao umri umewatupa mkono mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu na West Ham haina mpango wa kuwaongeza hivyo inataka kuwauza na kupata pesa badala ya kushuhudia wakiondoka bure.