BEKI wa kati, Virgil van Dijk amethibitisha kwamba Liverpool bado haijampa ofa ya mkataba mpya na hivyo kumfanya aingie kwenye miezi 12 ya mwisho ya dili lake kwenye kikosi hicho cha miamba ya Anfield.
Beki huyo Mdachi amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu kabisa kwenye kikosi hicho cha Liverpool kwa miaka ya hivi karibuni, akichangia mafanikio makubwa tangu alipojiunga Januari 2018, wakati kocha Jurgen Klopp alipovunja rekodi ya uhamisho kunasa saini yake.
Van Dijk sasa anaweza kuondoka bure kabisa itakapofika mwakani kutokana na Liverpool kutompa dili jipya.
Liverpool imekuwa ikisitasita kutoa mkataba mpya kwa beki huyo kutokana na umri wake, ambapo hana muda mrefu atafikisha umri wa miaka 33.
Kwa kawaida imekuwa ikitoa ofa ya mkataba wa mwaka mmoja tu kwa wachezaji wa aina hiyo, lakini kwa kesi ya Van Dijk bado haijafahamika mwisho wake kutokana na beki huyo kuendelea kucheza kwa kiwango cha juu.
Van Dijk ameonekana kuhuzunishwa na kitendo cha mkataba kutokuwa tayari na alisema kwenye mechi ya ushindi dhidi ya Sevilla kwenye pre season aliposema: “Bado hakuna mabadiliko yoyote hadi sasa.”
Kulikuwa na wasiwasi kwamba huenda Van Dijk angefungasha virago vyake na kuondoka Anfield wakati Klopp alipoamua kuachana na timu hiyo. Lakini, aliamua kubaki na timu hiyo, ambayo sasa inanolewa na Arne Slot.