Yanga itahitaji kusajili straika mwingine matata wa kuziba pengo la Heritier Makambo ambaye amesaini katika klabu ya Horoya ya Giinea, klabu hiyo ikiwa imebakiza mechi mbili mkononi dhidi ya Mbeya City na Azam FC.
Amefanya mengi ndani ya klabu hiyo, hilo linadhihirishwa na namna ambavyo alipata kibali mbele ya wadau wa soka nchini na umarufu mkubwa, uliotokana na kazi yake bora na staili ya maisha yake.
Mwanaspoti linakuleta mambo matano ambayo yatakumbukwa kutoka kwa Makambo hasa kwa staili zake alizoishi hapa Tanzania.
AINA YA USHANGILIAJI WAKE
Makambo alijitambulisha kwa mashabiki wake kwa aina ya ushangiliaji wake wa kupiga makofi kama anahitaji ujazo wa kitu fulani hivi, staili yake ilipamba kila kona na ilipata umarufu mkubwa mpaka kwenye mitandao ya kijamii, ikitumika na lika zote.
Yanga ilikuwa ikicheza ukisikia makofi basi ilikuwa inatambulisha kwamba Makambo kaishatupia.
Pia Soma
- Kumekucha fainali za AFCON, bei ya tiketi za ndege yatangazwa
- Mwadui kumenuka unaambiwa, wachezaji watishia kugoma
- Wachambuzi: Mfalme wa mabao Makambo amendokoka wakati sahihi
Mashabiki wa Yanga walikuwa wanapenda kuitumia staili ya Makambo, kuwakejeli watani wao wa Simba, pindi staa huyo akitupia, nje na hiyo pia alikuwa anashangilia kwa kuweka vidole kwenye masikio yote mawili, hizo ni kati ya alama alizoziacha kwa wadau wa soka Tanzania.
Nje na Yanga kuna baadhi ya wachezaji wa timu nyingine walikuwa wanaiga shangilia ya Makambo ya kupiga makofi ya ujazo, hilo liliwahi kutoke kwenye michuano ya Mapinduzi, Zanzibar.
Lakini nao Simba hawakuwa nyuma kutoa kejeli pindi mchezaji huyo akikosa kuzifumania nyavu, basi walikuwa wanapiga makofi ya ujazo ili kuwakera Yanga.
MIAKA 19
Achana na kashi kashi zake uwanjani, Makambo alikuwa na umri mdogo ambao ulikuwa unampa kasi zaidi ya kufanya makubwa uwanjani kama pumzi na kasi ya kuzisakama nyavu za wapinzani wake.
AMEIBEBA YANGA
Ameachana na Yanga, akiwa ameifanyia makubwa ana mchango wa kipekee kwani ndiye anayeongoza kwa mabao 16, ndani ya klabu hiyo na pengine yatabakia kuwa mtihani wa kuja kuvunja rekodi yake kwa msimu ujao dhidi ya washambuliaji wa timu hiyo.
Kwa mabao hayo, Makambo ameibeba timu yake kuwa nafasi nzuri ingawa bado ni kitendawili kama itaishia ya pili ama kuchukua ubingwa, hii itategemeana na kile watakachokipata watani wao Simba kwenye mechi zao nne na wao mbili ambazo wamebakiwa nazo dhidi ya Mbeya City na Azam FC.
Mbali na kufunga mabao 16, yalikuwemo yale yakuvutia zaidi, lakini pia alikuwa anatumia miguu yote miwili kwa maana wa kushoto na kulia kuhakikisha anacheza na nyavu.
UTUKUTU WAKE
Makambo alikuwa mtukutu licha ya muonekano wake ulikuwa hauungi mkono baadhi ya matukio ya kichokozi ambayo alikuwa anawafanyia timu pinzani na ilikuwa ngumu kwa mwamuzi husika kumpa adhabu ya kadi.
Alijitofautisha na wachezaji wengine ambao walikuwa wanacheza rafu za wazi ambazo zilikuwa zinawagharimu kama ilivyokuwa kwa kiungo wa timu hiyo, Fei Toto ambaye alikuwa anaadhibiwa mara kwa mara.
Kuna wakati waamuzi nao walikuwa wanaonja joto la jiwe pale ilipokuwa inatokea wachezaji wamewazunguka wengi kulalamikia baadhi ya vitendo ovu ndani ya uwanja, basi Makambo alikuwa anatumia mpenyo huyo kuwavuruga kama kuwakanyaga, ilikuwa ngumu kuonekana mpaka ilipokuwa inaonyeshwa na TV.
UPAMBANAJI WAKE
Yote katika yote Makambo alikuwa aina ya mchezaji ambaye alikuwa hakubali kushindwa hata kama timu imezidiwa uwezo alikuwa anapambana kuhakikisha wanatoka na pointi tatu.
Mfano kuna mipira ambayo ilikuwa inaelekea kufa, Makambo alikuwa anaifuatilia mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha anaimalizia kwa faida na sasa huduma yake hiyo wanaenda kuifaidi klabu ya Horoya ya Guinea.