Kiungo Jonas Mkude ameipeleka Simba hatua ya fainali baada ya kuifunguia penalti ya mwisho dhidi ya Kakamega ya Kenya kwenye mashindano ya SportPesa Super Cup yaliyofanyika leo Alhamisi.
KIPINDI CHA KWANZA
Simba ilitawala kipindi chote cha kwanza, ikitengeneza mashambulizi kutokea pande zote za uwanja, lakini haikuweza kupata bao.
Pamoja na Simba kutawala mchezo, Kakamega Homeboys ndio walikuwa wa kwanza kujaribu kuzitafuta nyavu za wapinzani wao lakini mashuti mawili ya Wafula Noah na Ahmed Ali yalipaa juu ya lango.
Simba ilicharuka kuanzia dakika ya 30-45, na kutengeneza mashamblizi matano ya maana lakini haikuweza kupata bao.
Ilianza kwa shuti la Shiza Kichuya kupaa katika dakika ya 35 kabla ya shuti la Haruna Niyonzima kupanguliwa na golikipa wa Kakamega Homeboys, Mauda Hedmond.
Chipukizi Rashid Juma nusura aipatie Simba bao katika dakika ya 38 lakini shuti lake lilidakwa kabla ya Mohammed Rashid kupoteza nafasi mbili za wazi kabla ya mpira kwenda mapumziko.
KIPINDI CHA PILI
Simba ilianza dakika 10 za kwanza za kipindi cha pili kwa kasi, na kutengeneza nafasi mbili kupitia kwa Rashid Juma lakini golikipa wa Kakamega, Mauda Hedmond alikuwa makini kuzuia hatari hizo.
Winga wa Kakamega, Noah aliinyima timu yake fursa ya kupata bao katika dakika ya 58 baada ya kugoma kumpasia Allan Wanga aliyekuwa ndani ya eneo la hatari na kuingia mwenyewe kisha kupiga shuti lililopanguliwa na kipa wa Simba, Aishi Manula.
Jonas Mkude alionyeshwa kadi ya njano katika dakika hiyo huku Simba ikimtoa Rashid Juma na kumpa nafasi Adam Salamba.
Kakamega walicharuka katika dakika ya 60-70 lakini juhudi za washambuliaji wao wawili, Mudavadi Mosses na Noah ziliishia mikononi mwa Manula.
Erasto Nyoni alipoteza nafasi ya kuifungia Simba bao la kuongoza dakika ya 70 kabla ya Mosses Kitandu aliyeingia kuchukua nafasi ya Mohammed Rashid kushuhuidia shuti lake likidakwa na kipa wa Kakamega, Hedmond dakika tano baadaye.
Mkude amefunga penalti hiyo ikiwa ni ya tano baada ya wachezaji wengine kama Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni Shomari Kapombe na Shiza Kichuya kutupia vyema wavuni penalti zao.