Dar es Salaam. Ni suala la muda lililobaki kwa Simba kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, baada ya jana kuilaza Ndanda ya Mtwara mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, mchezaji Meddie Kagere alivunja rekodi ya Emmanuel Okwi baada ya kufunga mabao mawili na kufikisha 22 msimu huu.
Msimu uliopita Okwi aliibuka mfungaji bora, baada ya kufunga mabao 20. Akizungumza Dar es Salaam jana, Kagere alisema siku zote amekuwa na kiu ya kufunga mabao katika kila mchezo wa Ligi Kuu.
“Napenda kufunga kila mchezo, leo nikifunga moja nataka mechi ijayo nifunge zaidi, hata wachezaji wenzangu wanajua. Siko hapa kushindana na mtu mimi nataka kuipa Simba mafanikio,” alisema Kagere.
Kagere ana nafasi kuwa mfungaji bora kwa kuwa wanaomfuata Salim Aiyee wa Mwadui na Heritier Makambo wa Yanga wana mabao 16 kila mmoja.
Kibarua cha kusaka pointi tano kufikisha 90 zitakazoipa ubingwa kimezidi kurahisishwa na ushindi huo ambao unaifanya kuhitaji pointi mbili tu katika mechi tatu ilizobakiza dhidi ya Singida United, Biashara United na Mtibwa Sugar. Pointi hizo 90 hazitafikiwa na timu yoyote ikiwemo Yanga hata kama itashinda mechi mbili dhidi ya Mbeya City na Azam kwa kuwa itafikisha pointi 89. Katika mechi ya jana presha ya Simba langoni mwa Ndanda ilianza mapema na kuzaa matunda ambako dakika ya tano ilipata bao lililofungwa na Kagere aliyeunganisha kwa kiki kali pasi ya nahodha wake John Bocco. Kagere alifunga bao la pili dakika ya 11 baada ya kumzidi ujanja kipa Diey Makonga. Ndanda itajutia nafasi ya dakika ya 65 baada ya Yusuph Mhilu kupiga krosi nzuri iliyokosa mtu wa kufunga na kumuacha kipa wa Simba, Aishi Manula akiokoa.
Pia Soma
- VIDEO: Zahera asimulia alivyokosa mamilioni
- Bondia Wilder amzimisha Breazeale sekunde 41 tu jukwaani
- Simba yaitekenya Ndanda mabao 2-0 ikibakiza pointi moja kutwaa ubingwa
Ndanda: walianza na Diey Makonga, Aziz Sibo, Yassin Salum, Augustino Nsata, Abdallah Mfuko, Enrick Nkosi, Hassan Maulid, Baraka Majogoro, Mohammed Mkopi, Vitalis Mayanga na Kigi Makasi.