Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zakaria Hans Poppe ameunganishwa kwenye kesi ya jinai inayowakabili Rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ lakini yeye akarejea nyumbani huku akiwaacha wenzake wakiendelea kusota rumande.
Aveva na Kaburu wamekuwa wakisota rumande tangu walipopandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 29, 2017 baada ya kukosa dhamana kutokana na kukabiliwa na makosa ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana.
Lakini Hans Poppe amerejea uraiani baada kuunganishwa kwenye kesi hiyo leo Jumanne, Oktoba 16, 2018, kwa kuwa mashtaka anayohusishwa nayo ni mashtaka ya jinai ya kawaida ambayo yanadhaminika.
Katike kesi hiyo ambayo washtakiwa wote wanne kwa ujumla wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 10, akiwemo mfanyabiashara Franklin Lauwo ambaye bado hajapatikana, Hans Poppe yeye anahusishwa katika mashtaka mawili tu ambayo ni kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uwongo.
Kwa kuwa mashtaka hayo yanadhaminika, wakili wake Augustine Shio ameiomba mahakama imwachie huru kwa dhamana mshtakiwa huyo na Hakimu Thomas Simba anayesikiliza kesi hiyo amekubaliana na maombi hayo baada ya upande wa mashtaka kueleza hauna pingamizi la dhamana dhidi yake.
Hans Poppe ameachiwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili ambao wamesaini bondi ya dhamana ya Sh15 milioni kila mmoja.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa, Oktoba 19, 2018 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo ambapo washtakiwa watasomewa maelezo ya mashahidi katika kesi hiyo.
Mashtaka yanayomhusisha Hans Poppe
Hans Poppe anahusishwa katika shtaka la saba la kughushi nyaraka, linalowahusu washtakiwa wote lakini likiwa shtaka la kwanza kwake.
Katika shtaka hilo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro amedai kati ya Machi 10 na Mei 30, 2016 washtakiwa wote kwa nia ya kughushi, walighushi nyaraka inayoonesha kuwa Klabu ya Simba ilinunua nyasi bandia kwa thamani ya Dola za Marekani 40,577 wakati wakijua kuwa si kweli.
Shtaka lingine linalomhusisha Hans Poppe ni shtaka la tisa la kuwasilisha nyaraka za uwongo.
Katika shtaka hilo, washtakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya Machi 10 na Mei 30, 2016, waliwasilisha nyaraka ya uwongo kuonesha kuwa Klabu ya Simba ilinunua nyasi bandia kwa thamani ya Dola za Marekani 40,577, wakati wakijua kuwa ni uwongo kinyume cha Sheria ya Kodi ya Mapato.
Mashtaka ya Hans Poppe yazua mvutano mahakamani