Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukuta Simba wamkosha Fadlu Davids

GSDJSDS Ukuta Simba wamkosha Fadlu Davids

Wed, 18 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ule ukuta wa Simba mnauzingatia lakini? Umeshaupiga mwingi kwenye ligi ukiwa haujaruhusu bao, kama haitoshi ukaendeleza ubabe huo kimataifa, hivyo hadi sasa beki Henock Inonga ni kama hakumbukwi tena.

Simba imecheza mechi mbili za ligi bila kuruhusu bao, ikacheza tena mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika ugenini dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya na bado haijaruhusu bao. Lakini imeruhusu bao moja katika Ngao ya Jamii ikicheza mechi mbili.

Ndani ya ubora huo, kuna kazi ya maana inafanywa na watu watano lakini kinara wa ubora huo ni Che Malone Fondoh.

Kwenye mchezo dhidi ya Al Ahli Tripoli, Che Malone ndiye aliyeongoza kwa kutibua mashambulizi mengi ya Waarabu hao.

Che Malone alifanya kazi kubwa akitibua mashambulizi sita lakini kubwa ni lile ambalo Waarabu hao wanalia hadi sasa na ilitakiwa wapewe penalti wakiamini mwamuzi aliwanyonga.

Achana na Che Malone, kuna Abdulrazack Hamza anayecheza pacha na Mcameroon huyo, naye anafuata nyuma akitibua mashambulizi matatu ya Waarabu hao.

Hamza ameendelea kuwa beki muhimu kwenye ukuta wa Simba akimsotesha nje beki wa kigeni Chamou Karaboue ambaye analazimika kusubiri nje apumzishwe au akacheze kwingine.

Kipa mpya wa Simba Moussa Camara na mabeki wake wa pembeni Shomari Kapombe upande wa kulia na nahodha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ anayecheza kushoto, wanafuata kila mmoja akizima mashambulizi mawili ya Al Ahli Tripoli.

Camara anawaacha kidogo Kapombe na Tshabalala kutokana na kucheza krosi mbili ambazo kama sio mikono yake mambo yangekuwa magumu.

Ukuta huo mara ya mwisho umeruhusu bao kwenye mchezo dhidi ya Yanga ambao ndiyo timu pekee iliyopata bao mbele ya wachezaji hao wanne wa ulinzi huku mbele yao kukiwa na kiungo mkabaji Deborah Fernandez Mavambo.

INONGA HOI

Mashabiki wa Simba na hata mabosi wao basi watachekelea hili, ni kwamba wakati ukuta wao ukiruhusu bao moja pekee katika mechi tano za kimashindano walizocheza msimu huu, beki wao wa zamani Henock Inonga kule aliko FAR Rabat ya Morocco ndani ya mechi tatu za mashindano amesharuhusu mabao matatu.

FAR Rabat ikicheza ugenini wikiendi iliyopita mchezo wa Kombe la Shirikisho imelazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya El Merreikh ya Sudan na mechi nyingine iliyoruhusu bao ni dhidi ya Yacoub El Mansour ikipoteza nyumbani kwa mabao 2-1 kwenye Kombe la Excellennce.

Mchezo pekee ambao FAR Rabat imeshinda bila kuruhusu bao ni dhidi ya Dicheira ambao walishinda kwa mabao 2-0 wa Kombe la Excellennce.

MSIKIE FADLU

Kocha wa Simba, Fadlu Davids akizungumzia ukuta huo alisema kumekuwa na maendeleo mazuri ya muunganiko wa mabeki wake ambao wanaendelea kuonyesha ubora mkubwa kwenye mechi zao.

“Mpaka Sasa nadhani eneo la ulinzi limeimarika vizuri, ukiangalia inaonekana kuna maelewano mazuri kwa watu wanaocheza pale, kadiri tunavyoendelea kupata mechi ngumu za mashindano zinasaidia kutuweka sawasawa,” alisema Fadlu.

Simba bado ina kazi kubwa ya kufanya katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli utakaochezwa Jumapili ya wiki hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Baada ya mchezo wa ugenini uliochezwa wikiendi iliyopita nchini Libya kumalizika kwa matokeo ya 0-0, sasa Simba inahitaji ushindi wa aina yoyote ingawa inapaswa kuwa makini kwani ikitokea sare ya mabao, itakuwa imekula kwao kwani itaondolewa kwa sheria ya bao la ugenini.

Katika kujiandaa na hilo, Kocha Fadlu amesema: “Matokeo ya 0-0 tukiwa tunarudi nyumbani inatutaka kuwa makini zaidi ya ilivyokuwa mechi ya kwanza kwani tunafahamu tukifanya makosa ya kuruhusu bao hasa tukiwa bado hatujapata mabao itatuweka kwenye presha kubwa.”

Chanzo: Mwanaspoti