Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tundu Lissu, Spika waanza kuchukuana mahakamani, Jaji aahirisha kesi kwa muda

71449 LISSU+PIC

Thu, 15 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mchuano wa kisheria baina ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai umeanza kunoga mahakamani baada ya mabishano ya kisheria kuanza kuibuliwa na kila upande katika shauri hilo.

Lissu amefungua maombi Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute  Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri la maombi maalum kwa lengo la kupata amri mbalimbali kuhusiana na uamuzi huo wa kuvuliwa ubunge.

Amri hizo kwa mujibu wa hati ya maombi na hati ya maelezo yake ni pamoja na Mahakama kumwamuru Spika Ndugai awasilishe mahakama taarifa ya kumvua ubunge, aliyoitoa bungeni ili iweze kuupitia na kisha iamuru kuutengua na kuutupilia mbali.

Nyingine ni Mahakama imwamuru Spika ampatie yeye Lissu nakala ya taarifa ya kumvua ubunge, amri ya  kusitishwa kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu, wa Chama cha Mapinduzi.

Maombi hayo yametajwa leo Alhamisi Agosti 15,2019 na mawakili wa Lissu wakiomba mwongozo wa mahakama ili waweze kuzungumzia ombi la kusimamishwa kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, lakini ombi hilo limepingwa na mawakili wa Serikali wakidai kwa sasa sio muda muafaka wa kuanza kulisikiliza.

Pia Soma

Pia, upande wa wajibu maombi wameomba muda wa siku nane waweze kuwasilisha hati ya kiapo kinzani pamoja na hati ya maelezo kinzani kabla ya maombi hayo kupangiwa siku ya kuanza kusikilizwa.

Wakili wa Serikali Mkuu, Vicent Tango amesema kwa kuwa shauri hilo linahusisha mhimili mwingine, yaani Bunge basi wanahitaji kupata muda wa kushauriana na Bunge (Spika) ili kuweza kuandaa kiapo kinzani.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa Lissu, Peter Kibatala ingawa amesema kuwa hana tatizo na wajibu maombi kuomba muda wa kuwasilisha hati ya kiapo kinzani lakini amesema muda wa siku nane walioomba ni mrefu sana kulingana na mazingira ya kesi hii, ambayo amesema inabidi isikilizwe na kuamriwa ndani ya siku 14.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Sirilius Matyupa ameiahirisha kwa muda ili kuandika uamuzi kama ombi hilo la kusimamishwa kwa uapishwaji wa mbunge huyo mteule lisikilizwe leo ama la.

Lissu ambaye ni mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yuko nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake, jijini Dodoma akitokea bungeni.

Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, huku alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba ya Tanzania.

Alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutokuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Katika hati ya kiapo chake  kinachounga mkono maombi hayo, wakili Muhgwai anaelezea mkasa mzima wa tukio na mazingira ya shambulizi dhidi yake na matibabu yake nje ya nchi huku akitaja viongozi wa Bunge na wa Serikali waliomtembelea akiwa kwenye matibabu Kenya na Ubelgiji.

Katika hati ya maelezo yake, anadai Spika wakati akichukua uamuzi huo hakumpa sababu za kuchukua uamuzi huo wa kumvua ubunge na kwamba alihukumiwa bila kupewa haki ya kusikilizwa.

Pia, anadai kuwa alishindwa kuwasilisha tamko kuhusu mali na madeni kwa kuwa alikuwa katika matibabu hospitalini nje ya nchi na kwamba Spika alikuwa anatambua na au alipaswa kutambua hivyo kuwa alijeruhiwa vibaya wakati wa mapumziko ya vikao vya Bunge.

Anasisitiza kuwa katika muda wa miaka saba ya utumishi wake kama mbunge alitekeleza wajibu na majukumu yake kikamilifu kwa kuhudhuria vikao na kushiriki katika mijadala mbalimbali ndani ya Bunge.

Katika hati ya dharura Lissu anaiomba mahakama hiyo isikilize na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka kwani vinginevyo, Miraji Mtaturu ambaye Julai 19 mwaka 2019  alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ataapishwa kushika wadhifa huo.

Hivyo anadai atakuwa ameathirika kwa kuwa atapoteza haki zake zote, kinga na maslahi yake yote yanayoambatana na wadhifa wake huo wa ubunge.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea

Chanzo: mwananchi.co.tz