Taarifa za Simba kusajili straika mpya kipindi hiki muda mchache kabla ya dirisha kufungwa kesho Alhamisi, zimeshtua wengi, lakini mshtuko zaidi umekuja kwa mchezaji mwenyewe ambaye anatajwa kumalizana na timu hiyo.
Leonel Ateba raia wa Cameroon kutoka USM Alger, ndiye anayetajwa kumalizana na Simba akipewa mkataba wa miaka miwili.
Straika huyo ana kibarua kigumu cha kuthibitisha Simba haijakosea kumsajili kutokana na takwimu zake za ufungaji kuonyesha hazijatofautiana sana na zile za Freddy Koublan na Steven Mukwala ambao kocha Fadlu Davids ameonyesha kutoridhishwa nao.
Simba ilikamilisha kwa haraka uhamisho wa Ateba kwa gharama zinazotajwa kufikia Dola 200,000 (Tsh538 milioni) baada ya kufikia makubaliano na USM Alger ya Algeria ambayo mshambuliaji huyo wa Cameroon ameichezea kwa miezi sita tu tangu alipojiunga nayo kutokea Union Douala, Januari mwaka huu.
Katika kipindi cha nusu msimu alichoitumikia USM Alger, Ateba amecheza mechi 19 za timu hiyo ya Algeria. Ameifungia mabao matatu tu huku akitoa pasi nane za mwisho katika mashindano tofauti ambayo imeshiriki.
Kabla ya hapo, katika nusu msimu aliochezea Douala, Ateba aliifungia mabao saba hivyo kiujumla msimu uliopita alipachika mabao 10.
Freddy Koublan, katika nusu msimu uliopita alipochezea Simba, aliifungia mabao nane, sita yakiwa kwenye ligi na mawili ya mashindano mengine lakini kabla ya hapo, katika ligi ya Zambia alikotoka, kwa nusu msimu alipachika mabao 11 na hivyo kwa msimu uliomalizika alifunga mabao 19, tisa zaidi ya yale ya Ateba.
Kwa msimu uliopita, Mukwala katika Ligi ya Ghana alifunga idadi ya mabao 14 katika michezo 28 na hivyo anamzidi Ateba kwa mabao manne.
Msimu ambao Ateba alikuwa moto wa kuotea mbali katika ufungaji ni 2020/2021 ambapo aliifungia Coton Sports mabao 13 na kupiga pasi saba za mwisho katika mechi 28 na baada ya hapo hajawahi kufunga zaidi ya mabao 10 kwa msimu mmoja.
Lakini mbali na kuthibitisha kuwa Simba haikukosea kutumia kiasi kikubwa cha fedha kumsajili, Ateba anakabiliwa na kibarua kigumu cha kumaliza nuksi ya misimu mitatu mfululizo ambayo imewakumba washambuliaji wa kati wa Simba.
Kuanzia msimu wa 2021/2022 hadi uliopita wa 2023/2024, washambuliaji wa kati wa Simba wameonekana kuwa na ubutu jambo ambalo limeilazimisha timu hiyo kuingia sokoni kusajili mchezaji wa nafasi hiyo katika kila dirisha la usajili.
Kwa misimu mitatu iliyopita, hakuna mshambuliaji wa kati wa Simba ambaye alifanikiwa kufunga zaidi ya mabao 10 kwenye ligi.
Katika msimu uliopita, mshambuliaji wa kati wa Simba aliyepachika mabao mengi alikuwa ni Jean Baleke ambaye alifumania nyavu mara nane na alipoondoka katika dirisha dogo, aliletwa Koublan aliyefunga mabao sita.
Msimu wa 2022/2023, mshambuliaji wa kati wa Simba aliyefumania nyavu mara nyingi alikuwa ni Moses Phiri aliyemaliza akiwa na mabao 10 akifuatiwa na John Bocco aliyefunga mabao tisa.
Katika msimu wa 2021/2022, Meddie Kagere ndiye alimaliza akiwa kinara kwa upande wa washambuliaji wa kati ambapo alifunga mabao saba.
Msimu wa mwisho kwa washambuliaji wa kati wa Simba kutamba ulikuwa ni 2020/2021 ambao John Bocco alipachika mabao 16 na aliyemfuatia alikuwa ni Chris Mugalu aliyefunga mabao 15.
Fadlu amesema ni matakwa yake kuongezwa kwa mchezaji huyo kutokana na ubutu wa safu ya timu hiyo licha ya kutengeneza nafasi nyingi.
Wakati huohuo, amesema anafurahishwa na ubora wa beki Che Malone Fondoh ambaye amemtaja kuwa ni mchezaji kiongozi anayeweza kumsaidia kujenga kikosi bora kutokana na uzoefu wake kikosini na kuwa mzungumzaji mzuri awapo kwenye majukumu yake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Davis alisema anafurahia kuimarika kwa kikosi chake siku hadi siku huku akibainisha kwamba eneo la ushambuliaji limekuwa likishindwa kutumia nafasi licha ya kutengeneza nyingi lakini hana wasiwasi kwani ni shida ya muda tu.
“Kwa maandalizi tuliyofanya na mechi tulizocheza kikosi changu kimeimarika sana, naridhishwa na vijana wangu wanafuata maelekezo yangu kuna shida ndogo ndogo ambazo naamini zitatatuliwa kwa muda na kuwa na kikosi bora na shindani,” alisema na kuongeza;
“Ujio wa Mshambuliaji mpya utakuwa chachu ya ushindani na kuendelea kumuimarisha Karabaka ambaye naamini atakuja kuwa mshambuliaji tishio hapo baadae kutokana na umri wake na amekuwa akiimarika siku hadi siku.”
Davis alisema mechi za ngao ya jamii dhidi ya Yanga na Coastal Union zimeongeza kitu kikosini kwake na kumuonyesha mapungufu kabla ya mechi za ligi na michuano ya kimataifa kuanza.
“Kabla ya mechi na Yanga na Coastal Union tulikuwa na mechi za kirafiki mfululizo lengo lilikuwa ni kutafuta utimamu wa mwili kwa wachezaji wangu ambao kwa asilimia kumbwa wapo fiti na wanaendelea kuimarika siku hadi siku,” alisema na kuongeza;
“Kiujumla timu ipo tayari kwa mashindano na maeneo mengine ambayo yanakasoro ndogo ndogo naendelea kuyafanyia kazi kabla ya mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Tabora United Agosti 18 mchezo ambao nahitaji matokeo ili kuiweka timu yangu kwenye hali nzuri ya ushindani.”Nini maoni yako?