Washambuliaji Wazir Junior, Clement Mzize na Cyprian Kachwele wana jukumu kubwa la kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars katika mchezo wa leo kuanzia saa 1:00 usiku dhidi ya Guinea utakaochezwa Uwanja wa Charles Konan Banny uliopo Yamoussoukro nchini Ivory Coast.
Guinea ambayo imeamua kutumia uwanja huo kwa mechi zake za nyumbani baada ya nchini kwao kukosa kiwanja chenye sifa kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), leo itaingia uwanjani ikiwa imetoka kupoteza kwa bao 1-0 ugenini dhidi ya DR Congo katika mchezo uliopigwa Ijumaa iliyopita pale Stade des Martyrs, Kinshasa nchini DR Congo, huku Stars yenyewe ikiwa iliambulia suluhu nyumbani dhidi ya Ethiopia.
Rekodi zinaonyesha kwamba, Guinea imepoteza mechi mbili mfululizo kwa matokeo ya 1-0, kabla ya hapo ilikuwa imeshinda mechi tatu mfululizo kwa matokeo ya jumla ambapo ilifunga mabao 13 na kuruhusu mawili katika kipindi cha mwezi Machi na Juni mwaka huu, hivyo mchezo wa leo wataingia kwa hasira kubwa kuirekebisha rekodi yao mbovu.
Kwa upande wa Taifa Stars ambayo inaisaka Afcon ya nne tangu mwaka 1980, nayo haipo kinyonge kwani inatambua kwamba kushindwa kuondoka na pointi tatu leo itawaweka katika mazingira magumu ya kufuzu kwani hivi sasa ina pointi moja.
Stars ina kazi kubwa ya kufanya katika mchezo wa leo kwani tangu mwaka 2024 uanze, imeshinda mechi tatu pekee kati ya 11 za kimashindano na kirafiki huku ikifunga mabao saba kupitia washambuliaji wanne, Kelvin John, Wazir Junior, Oscar Adam na Ibrahim Hamad Hilika, wakati Simon Msuva ambaye ni kiungo mshambuliaji kama ilivyo kwa Abdul Suleiman Sopu kila mmoja akifunga moja sawa na beki Novatus Dismas.