Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene anatarajiwa kuzindua harambee ya Kampeni ya GGM Kili Challenge kwa mwaka 2022 inayoratibiwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini na kushirikisha wadau kuchangia mwitikio wa Taifa dhidi ya virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI.
GGM Kili challenge ni mfuko ulioanzishwa mwaka 2002 na kampuni ya GGM. Kampeni hii inasimamiwa na GGM kwa kushirikiana na TACAIDS ikiwa na lengo la kukusanya fedha ili kuisaidia serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia malengo ya sifuri tatu.
Malengo ya sifuri tatu yanamaanisha kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro jana, Mkuu wa mkoa huo, Steven Kagaigai alisema harambee inatarajiwa kuzinduliwa tarehe 14 Julai, 2022 katika hotel ya Weruweru River Lodge iliyopo wilayani Hai mkoani humo.
Alisema uchangiaji wa fedha hizo unalenga zaidi jamii zilizoko kwenye mazingira hatarishi ya maambukizi ya VVU na kupunguza athari za UKIMWI.
Alisema kampeni hiyo hufanyika kila mwaka na ilianza rasmi tangu mwaka 2002 na huu ni katika mwendelezo wa ukusanyaji fedha kwa ajili ya mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini sambamba na kutoa fursa ya utalii katika mlima Kilimanjaro.