SERIKALI imesema itaongeza nguvu ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya hususani kwa vijana ambao ni nguvu kazi kwa Taifa.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene alisema hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye Maadhimisho ya Siku ya Dawa za Kulevya Duniani iliyofanyika jijini Dodoma.
Simbachawene alitoa maagizo sita katika kupambana na dawa za kulevya na kutaka waraibu wa dawa hizo wapewe mitaji baada ya kurudi katika hali zao za kawaida.
Aliagiza kutoa elimu kwa wanahabari waweze kutoa mchango mkubwa katika kielimisha wananchi kupitia maandiko na vipindi vya redio na televisheni.
Pia asasi zisizo za kiserikali zinazofanya kazi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kutoa elimu jamii isijiingize kwenye matumizi .
Maagizo mengine ya serikali ni kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa elimuna viongozi wa dini kukemea matumizi ya dawa za kulevya.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolonia imetakiwa kuboresha mitaala kuwezesha vijana kupata elimu juu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya.
Waziri Simbachawene alisema tatizo la matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa huku bangi ikiongoza kwa kuwa na watumiaji wengi ikifuatiwa na heroin na cocaine ambazo huingia kutoka nje ya nchi.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Gerald Kusaya alisema Mamlaka imekamata watuhumiwa 12,549 na kati ya hao, 10 ni kuhusiana na cocaine, 605 heroin, 10,282 bangi na watuhumiwa 1,555 ni wa mirungi.