Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye Alhamisi alitangaza kuwa amelivunja bunge linaloongozwa na upinzani na kuitisha uchaguzi mpya wa bunge tarehe 17 Novemba.
“Nimelivunja bunge la taifa ili kuwaomba wananchi huru kupitia njia za kitaasisi ambazo zitaniruhusu kufanya mabadiliko ya kimfumo niliyowaahidi,” Faye alisema kwenye televisheni ya taifa.
“Leo kuliko hapo awali, wakati umefika kufungua awamu mpya katika muhula wetu,” alisema kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 44.
Faye alipata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa rais wa Mwezi Machi mwaka huu kwa ahadi ya kufanya mabadiliko makubwa katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Lakini hatua za serikali yake zimedumazwa na ukosefu wa wingi wa wabunge katika bunge la nchi hiyo.
Kulingana na katiba ya Senegal, Faye anaruhusiwa kulivunja bunge linalotawaliwa na upinzani kuanzia Septemba 12 na kuitisha uchaguzi wa mapema, ambao utamuwezesha kupata wingi wa wabunge unaohitajika ili kutekeleza ajenda yake.