Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Michael Owen ametabiri Arsenal kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England (EPL) msimu ujao wa 2024/2025 huku akishindwa kuiweka Man United katika orodha ya timu nne zitakazomaliza katioka nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Owen ambaye pia amewahi kuichezea Liverpool, anaamini kuwa Arsenal itazima ubabe wa Man City na kutwaa ubingwa wa EPL baada ya kuukosa msimu uliopita ilipozidiwa kwa pointi mbili mwishoni mwa msimu.
Katika utabiri wake alioutoa katika mtandao wa EPL jana, Owen ameiweka Liverpool kumaliza katika nafasi ya pili, Aston Villa kumaliza katika nafasi ya tatu na Man City kumaliza katika nafasi ya nne.
Utabiri wa Michael Owen kuwa Arsenal itachukua ubingwa wa EPL, umefanana na ule wa nyota wa zamani wa Tottenham Hotspur, Darren Bent ambaye naye anaamini kitu kama hicho.
Hata hivyo Bent ametofautiana na Owen katika nafasi tatu zinazofuata kwenye msimamo ambapo yeye ametabiri nafasi ya pili kuchukuliwa na Man City, Liverpool kuwa nafasi ya tatu na ile ya nne kuchukuliwa na Chelsea.