Taarifa ambazo tunazo zinabainisha kwamba Mchezaji wa Simba Fabrice Ngoma anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji maisha yake yanaweza yasiwe marefu klabuni hapo baada ya kuwepo kwa ofa kutoka timu mbalimbali zikimuhitaji.
Ngoma kwa sasa nafasi yake inaonekana finyu ndani ya Simba chini ya Kocha Fadlu Davids, anayeamini zaidi katika vijana, kiungo huyo anashindania namba dhidi ya Augustine Okejepha, Debora Fernandes, Mzamiru Yassin na Yusuf Kagoma, jambo linalooneka linamtoa mchezoni.
Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kwamba wakala wa mchezaji huyo, Faustine Mukandila yupo hapa nchini na juzi Jumapili alikuwepo Uwanja wa Benjamin Mkapa, kushuhudia mechi za Ngao ya Jamii, imeelezwa ana mpango wa kuzungumza na Simba kuhusiana na suala hilo.
“Kuna timu ya Saudia na Qatar ambazo zimepeleka pesa ndefu, ilionekana kushindikana viongozi wakiamini bado ana umuhimu wa uwepo wake kikosini, wakiamini ni kiongozi mzuri dhidi ya wengine na ndiye mwenye CV kubwa dhidi ya wenzake,” kilisema chanzo.
Kabla ya hapo, iliwahi kuelezwa Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi aliwahi kuvutiwa na huduma ya Ngoma, ingawa hakufanikiwa kuinasa saini ya kiungo huyo ambaye amebakiza mkataba wa mwaka mmoja ndani ya Simba.