Balaa hilo. Mashtaka 115 yanayoikabili Manchester City juu ya madai ya kuvunja kanuni za ukomo wa matumizi kwenye Ligi Kuu England yataanza kusikilizwa mwezi ujao, huku ikielezwa hukumu yake inaweza kutoka mapema kabisa Mwaka Mpya 2025.
Ripoti zinafichua wakati ikitarajiwa kamati huru inayosimamia kesi hiyo ikitarajiwa kukutana Novemba, kinachoelezwa kwa sasa ni mashtaka hayo yataanza kusikiliwa katikati ya Septemba kama hakutakuwa na ucheleweshwaji wowote wa kisheria.
Mashtaka hayo yanaweza kusikilizwa kwa muda wa zaidi ya wiki 10, huku kila kesi itaamriwa kivyake kisheria kutokana na madai ya Man City kwenye utetezi wao wa kuhusu miamala iliyokuwa ikifanyika kwenye kipindi cha usajili wa wachezaji.
Man City inakanusha kufanya makosa juu ya madai kwamba ilifanya udanganyifu kwenye matumizi ya pesa za usajili, kwamba kulikuwa na pesa zisizotokana na mapato ya mpira zilikuwa zikiingizwa kwenye matumizi ya miamba hiyo.
Kitu ambacho kinawakabili Man City, endapo kama watakutwa na hatia basi hatari yake ni kushushwa daraja na adhabu nyingine kali zitakazotolewa na Ligi Kuu England ikiwamo kupokwa pointi.
Man City inadaiwa kufanya udanganyifu huo kwenye misimu tisa tofauti na inaelezwa klabu hiyo ilikuwa inashindwa kuweka bayana usahihi wa hesabu zao za kifedha na malipo iliyokuwa ikifanya timu hiyo, wakati inamlipa Kocha Roberto Mancini na baadhi ya wachezaji.
Man City imefunguliwa mashtaka pia kutokana na kushindwa kutoa ushirikiano kwenye kipindi cha upepelezi wa sakata hilo.
Alipozungumza Aprili mwaka huu, mkurugenzi mtendaji mkuu wa Ligi Kuu England, Richard Masters alisema majibu ya kesi hiyo yatapatikana hivi karibuni. Man City iliajiri kampuni ya uwakili ya Lord Pannick KC kwenye ishu ya kujitetea na imeendelea kukazia haijafanya kosa.
Man City ilifungiwa kucheza michuano ya Ulaya na shirikisho la soka barani humo UEFA kwa kipindi cha miaka miwili mwaka 2019, lakini adhabu hiyo iliondolewa baada ya timu ya Etihad kukata rufaa.
Ligi Kuu England ilianza uchunguzi wa suala hilo mwaka mmoja kabla ya chapisho la Football Leaks kwenye tovuti moja ya Ujerumani, Der Spiegel na iliweka wazi masilahi yaliyokuwa kwenye mkataba wa Mancini na makbaliano ya malipo ya haki za taswira za mchezaji Yaya Toure na barua pepe iliyofichua kwamba pesa ya udhamini ya kuwalipa watu hao ilikuwa ikitoka moja kwa moja kwa mmiliki wa timu.
Katika kila msimu kuanzia 2009/10 hadi 2017/18, Ligi Kuu England ilikuja na kanuni ya kuzitaka klabu kuweka wazi vyanzo vyao vyote wa kifedha na matumizi yanayofanyika kwenye timu hiyo ili kuweka usawa, kukwepa ishu ya kuingiza pesa haramu kwenye mchezo huo wa soka.
Mashtaka hayo yatasikilizwa kwa usiri mkubwa kutokana na kanuni za Ligi Kuu England na mwisho kabisa kamisheni huru itaweka chapisho la hukumu kwenye tovuti ya Ligi Kuu England.
MECHI 10 ZA KWANZA
ZA MAN CITY KWENYE
EPL MSIMU WA 2024/25
-Agosti 18 vs Chelsea (ugenini)
-Agosti 24 vs Ipswich Town (nyumbani)
-Agosti 31 vs West Ham (ugenini)
-Septemba 14 vs Brentford (nyumbani)
-Septemba 22 vs Arsenal (nyumbani)
-Septemba 28 vs Newcastle (ugenini)
-Oktoba 5 vs Fulham (nyumbani)
-Oktoba 20 vs Wolves (ugenini)
-Oktoba 26 vs Southampton (nyumbani)
-Novemba 2 vs Bournemouth (ugenini)