Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amewalaumu viongozi wa zamani na wakoloni kwa umaskini wa Uganda na kusema walitia sumu akili za wakulima wanaofanya kazi kwa bidii.
Museveni amesema hayo alipokuwa akiwahutubia viongozi kutoka kanda ndogo ya Acholi na Lango katika jimbo la Baralegi wilayani Otuke.
“Wakoloni walipokuja hapa waliwafanya watu wetu walime mazao wanayoyataka, pamba, tumbaku, kahawa, chai, halafu viongozi wetu waliiga tu walichoambiwa na wakoloni. Kwa hiyo nilipochunguza suala hilo niliona, hatari namba moja ilikuwa ni kufanyia kazi tumbo tu,” amesema Rais Museveni.
Aidha, amewahimiza Waganda walioathirika na umaskini kuchagua kwa uangalifu biashara nzuri kama vile kahawa, matunda, ng’ombe wa maziwa, ufugaji wa nguruwe, kuku na samaki. Pia kuchagua makampuni yenye mahitaji makubwa ndani ya uganda, Afrika na kimataifa.
Hata hivyo, amewakumbusha wakulima kuhusu vanila ambayo ilikuwa na soko zuri, na kusema kuwa watu waliokuwa wakiikuza hawakuangalia mahitaji ya kimataifa.
Mwaka 2021, Wizara ya Fedha ya Uganda iliripoti kwamba asilimia 28 ya Waganda walikuwa maskini. Wizara ya Fedha pia ilibaini kuwa theluthi mbili ya Waganda wamepoteza mapato kutokana na janga la UVIKO19.