TUME ya Taifa ya Uchaguzi Uganda imemteua Rais Yoweri Museveni kuwa mgombea wa urais kupitia chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.
Rais Museveni aliyeongoza nchi hiyo tangu mwaka 1986, alishukuru kwa uteuzi huo na kutaka wananchi kulinda amani kwani anasikia kuna wanaotaka kuanzisha machafuko, akisema hakuna wa kuitisha Uganda.
“Mimi Jaji Simon Byabakama ninamtangaza Yoweri Kaguta Tibuhaburwa Museveni kuwa mgombea urais aliyeteuliwa kwa haki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021,” alisema Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Simon Byabakama.
Tume ilieleza kuwa Museveni aliteuliwa jana asubuhi na kufuatiwa na Henry Tumukunde (mgombea binafsi), John Katumba (mgombea binafsi), Mugisha Muntu (Alliance for National Transformation) na mgombea binafsi Nancy Kalembe.
Uteuzi Museveni umefanyika huku kukiwa na ulinzi mkali kwenye Jiji la Kampala, huku polisi wakitoa onyo kwa wananchi kufanya maandamano kwa askari wakitanda katika maeneo mbalimbali.
Baada ya uteuzi huo, Museveni (76) alitaka kuwepo kwa amani na usalama na yeyote atakayejihusisha na vurugu atakabiliwa vikali.
“Nataka kuwashukuru wanachama wa NRM katika wilaya zote walionidhanini kwani nilitakiwa kupata takribani saini mia moja lakini nilipata zaidi na mchana huu tutaenda kuzindua ilani yetu,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe.