RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni amesema suluhisho la migogoro ya kisiasa Sudan Kusini ni kufanyika kwa uchaguzi hali itakayosaidia kutatua matatizo ya kisiasa yaliyopo.
Amesema uchaguzi utalazimisha wanasiasa katika taifa hilo kutengeneza umoja kama ilivyofanya Kenya na hivyo kuleta amani na usalama nchini humo.
Rais Museveni alisema hayo wakati akizungumza na ujumbe maalumu kutoka nchi za mjini Jinja juzi.
“Dawa ya kweli ya matatizo ya Sudan Kusini ni kufanyika kwa uchaguzi mkuu kwani tatizo kama hilo lilikuwapo Kenya lakini walipata ufumbuzi baada ya kufanyika kwa uchaguzi hivyo nawaomba viongozi wa Sudani Kusini kuangalia namna ya kufanya uchaguzi,” alisema.
Rais huyo wa Uganda alisema nchi hiyo ikifanya uchaguzi wanasiasa wataunda umoja na matatizo yote yatakuwa historia.
Katika mkutano huo, Balozi wa Marekani nchini Uganda, Natalie Brown aliongozana na mjumbe maalumu wa Marekani Sudan Kusini, Stuart Symington, huku Balozi wa Uingereza nchini Uganda, Kate Airey akiongozana na mjumbe maalumu wa Uingereza nchini Sudan Kusini, Robert Fairweather.
Ujumbe huo ulifika kumtaarifu Rais Museveni kuhusu hali ya kisiasa Sudan Kusini na hali inavyoendelea katika kuhakikisha kunakuwa na amani na usalama wa kudumu.