RAIS Yoweri Museveni ameipongeza Tanzania kwa mwelekeo wa maendeleo ya kiuchumi ya uzalishaji mali yanayogusa si tu maisha ya Watanzania, bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki katika utoaji wa huduma.
Alisema mwelekeo huo wa uzalishaji mali kwa kutumia rasilimali zenye ukomo ili wananchi wapate huduma bora, ni mambo ambayo alikuwa wakiyazungumza mara nyingi na Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.
Rais Museveni aliyasema hayo juzi Ikulu, Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini Mkataba wa Nchi Hodhi (HGA) wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki uliofanywa kati ya Tanzania (nchi mwenyeji) na Kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP).
Hafla hiyo ilishuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais Museveni, viongozi wa kampuni za uwekezaji wa mradi huo ikiwemo Kampuni ya Total, Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Taifa la Mafuta la China (CNOOC), viongozi wa serikali na wa sekta binafsi.
Rais Museveni alisema mataifa mengi ya Afrika yanapata shida katika mwelekeo ndio maana kunakuwa na shida katika utoaji wa huduma kwa jamii na wananchi wamekuwa wakizilalamikia serikali zao bila kujua kuwa hakuna huduma bora bila uzalishaji mali, hatua ambayo sasa Tanzania inaifanya.
“Naamini huko aliko Mwalimu Nyerere anafurahi kuona mafanikio hayo kwani kwa miaka 60 niliyoshiriki katika harakati za ukombozi na maendeleo ya Ukanda wa Afrika Mashariki, nimegundua kuwa tatizo kubwa la nchi za Afrika ni kukosa muelekeo ili kupata ustawi wa jamii,” alisema Rais Museveni.
Mhitimu huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema sasa anauona mwelekeo kupitia ushirikiano huo wa Tanzania na Uganda katika kutumia rasilimali zinazoisha kama mafuta, gesi na madini kwa ajili ya kuimarisha sekta zianzodumu kama kilimo na huduma kwa wananchi jambo alilokuwa akiliongea na Mwalimu Nyerere mara nyingi.
Alisema hakuna huduma bila uzalishaji mali na uzalishaji mali unategemea sekta nne alizozitaja kuwa ni kilimo cha biashara, viwanda, huduma (usafiri, benki, muziki) na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Rais wa Kampuni ya Total wa Utafiti na Uzalishaji Afrika, Nicolas Terraz alisema mradi huo ni hatua mpya ya ushirikiano mkubwa kwa nchi za Afrika Mashariki ambao Tanzania itapata Dola za Marekani bilioni nne (zaidi ya Sh trilioni tisa).
Rais wa Kampuni ya CNOOC Uganda Ltd, Chen Zhuobiao alishukuru kwa kupata heshima ya kushiriki katika tukio hilo la kihistoria kama mmoja wa wanahisa.
Alisema ana matumaini watafanyakazi kwa ushirikiano mkubwa na wabia wengine na serikali zote mbili (Uganda na Tanzania) ili kufikia mwishoni mwa mwaka 2024 ujenzi uwe umekamilika na mafuta yaanze kusafirishwa mwaka 2025.
Katika hafla hiyo, pia marais hao walisaini mkataba wa makubaliano ya Tamko la Pamoja la utekelezaji wa mradi huo lililosomwa kwa niaba yao na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Liberata Mulamula.