Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Museveni anavyoimarisha familia yake serikalini

Museveni Janeth Museveni anavyoimarisha familia yake serikalini

Fri, 22 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Yoweri Museveni wa Uganda baada ya kuweka rekodi kuwa Rais wa kwanza barani Afrika kumteua mkewe Janet kwenye Baraza la Mawaziri, amevunja rekodi hiyo kwa kumteua mwanaye Muhoozi Kainerugaba kuwa Mkuu wa Majeshi.

Jenerali Muhoozi ni mzaliwa wa Dar es Salaam nchini Tanzania Aprili 24, 1974 kwa wazazi, Museveni na Janet. Museveni mwenye umri wa miaka 79 alizaliwa Ntungamo nchini Uganda Septemba 15, 1944 na yuko madarakani tangu mwaka 1986.

Mbali na uteuzi wa Muhoozi na mkewe Janet, Museveni pia ana rekodi ya kuteua familia na jamaa zake kwenye nafasi za kadhaa serikalini, mdogo wake Jenerali Caleb Akandwanaho au Salim Saleh kama anavyofahamika naye alikuwa ana nafasi kubwa jeshini na kwenye siasa.

Uteuzi wa Jenerali Muhoozi umefanyika jana akichukua nafasi ya Jenerali Wilson Mbasu Mbadi ambaye ameteuliwa kuwa Waziri Nchi anayeshughulikia Biashara. Muhoozi kabla ya uteuzi huo alikuwa mshauri mwandamizi wa Rais kwa shughuli maalumu, pia Museveni ambaye cheo chake cha kijeshi ni jenerali, amemteua Luteni Jenerali Samuel Okiding kuwa mkuu wa majeshi msaidizi, akichukua nafasi ya Jenerali Peter Elwelu ambaye anakuwa mshauri mwandamizi wa Rais.

Kuteuliwa kwa Muhoozi kunaelezwa ni njia ya kuelekea kumrithi baba yake kwenye nafasi ya Rais wa Uganda na hasa kutokana na jumbe zake kwenye akaunti yake ya X zamani Twitter, yenye wafuasi zaidi ya 650,000 kwamba yeye ndiye Rais ajaye wa Uganda.

Muhoozi amekuwa akitoa tambo nyingi kwenye akaunti yake hiyo ikiwamo anaweza kuiteka Kenya ndani ya wiki mbili, kwamba Waafrika wote wanaunga mkono kitendo cha Russia kuivamia Ukraine.

Pia, alitangaza kutoa mahari ya ng’ombe 100 kwa ajili ya kumuoa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke nchini Italia, Giorgia Meloni anayeshika wadhifa huo tangu Oktoba 2022.

Lakini, pia aliendelea kuweka wasifu wake kwenye akaunti ya X akijaribu kuonyesha ubora wake wa kumrithi baba yake kwenye nafasi ya urais. Pia, aliwahi kutamka kuwa akiwa Rais ataongeza bajeti ya michezo.

Muhoozi pia amewahi kutwiti akiunga mkono waasi wa Tigray wanaopigana na majeshi ya Serikali ya Ethiopian, pia aliwahi kutwiti akiunga mkono waasi wanaofanya mapigano huko mashariki mwa Congo.

Waganda wanamuona Muhooza kama jenereta lililo tayari kuwaka umeme unapozimika, kwa maana yuko tayari akisubiri kuchukua madaraka ya nchi pale baba yake atakapoachia ngazi. Uchaguzi wa Rais wa Uganda utafanyika mwaka 2026.

Pia, amelaumiwa kwa kitendo chake cha hivi karibuni cha kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa akizunguka nchi nzima, wakati maofisa wa jeshi hawaruhusiwi kushiriki siasa.

Hata hivyo, Muhoozi alijitetea anachofanya ikiwamo kuzindua kikundi cha kuhamasisha uzalendo wa Uganda kwamba siyo siasa na wala kikundi hicho hakihusiki na chama chochote cha siasa zaidi ya kuhamasisha uzalendo.

Museveni ambaye alichukua nchi mwaka 1986 amechaguliwa mara sita na hajatamka lini anastaafu uongozi wa nchi, amewahi kutajwa na chombo cha habari ‘The Independent’ kuhusu kinachoitwa ‘Museveni government’s Family Tree’ kwa maana familia yake ilivyojazana serikalini.

Kwa mujibu ‘The Independent’ kwenye toleo lake la miaka kadhaa iliyopita lilitaja wanafamilia wa Museveni waliomo serikalini, kwenye siasa, jeshini na maeneo mengine.

Baadhi ya wanafamilia viongozi

Mdogo wa Museveni, Jenerali Caleb Akandwanaho ambaye pia anafahamika kwa jina la Salim Saleh. Ni mstaafu wa vita vya msituni na amekuwa na ushaushwi kwenye jeshi na idara ya usalama, alikuwa Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya fedha, baadaye aliteuliwa kuwa mshauri wa Rais kwenye masuala ya ulinzi.

Janet Kataha Museveni: Ni mke wa Museveni ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruhaama na Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Karamoja. Pia, kwa kutumia kivuli cha mumewe ana ushawishi mkubwa kwa wabunge wa NRM. Wakati wa kashfa ya ardhi ya Temangalo alimtaka Waziri wa Usalama, Amama Mbabazi ajiuzulu wadhifa wake au arejeshe fedha kiasi cha Sh11 bilioni. Miriam Karugaba: Ni dada wa Museveni ambaye ni ofisa utawala Ikulu.

Natasha Museveni Karugire: Ni binti mkubwa wa Rais Museveni ni msaidizi mkuu anayesimamia masuala ya ikulu iliyopo Entebbe.

Dk Joseph Ekwau: Ni mtoto wa dada wa Rais Museveni, Dk Violet Kajubiri. Dk Ekwau ni mshauri wa Rais masuala ya mifugo.

Jimmy Karugaba: Ni mume wa dada wa rais Museveni Miriam Karugaba. Ni ofisa msimamizi wa idara ya uhasibu ikulu.

Meja Bright Rwamirama: Ni Waziri wa Kilimo na pia mbunge wa Isingiro Kaskazini. Rwamirama ni mpwa wa Museveni.

Shedrack Nzeire: Ni kaka wa kambo wa Museveni na amekuwa mhamasishaji wa vijana Ikulu.

Faith Katana Mirembe: Ni mpwa wa Museveni ambaye ni katibu binafsi msaidizi wa Rais Museveni anayehusika na masuala ya elimu na huduma kwa jamii.

Amelia Kyambadde: Ni katibu mkuu binafsi kwenye ofisi ya Rais Museveni. Ni mjukuu wa Meja Murari Kafureka ambaye ana uhusiano na Rais Museveni kupitia kwa Sam Kutesa. Mpwa wao Albert Muganga alimuoa Ishta ambaye ni dada wa mke wa Muhoozi, Charlotte Kutesa.

Meja Sabiiti Magyenyi: Ni mpwa wa Rais Museveni ambaye ndiye kamanda mkuu wa kikosi kinachomlinda Rais. Anaelezwa alijiunga jeshi kwa ushawishi wa Muhoozi na alicha kuendelea na masomo yake ya shahada ya uzamivu huko Uingereza ili ajiunge jeshi.

Kanali Kateera: Ni mpwa wa mke wa Museveni, Janet Museveni, ni kamanda divisheni ya nne huko Gulu. Aliwahi kufanya kazi kwenye idara ya fedha jeshini. Luteni Allan Matsiko: Ofisa upelelezi Ikulu na ni kaka wa Albert Muganga pia ni mpwa wa mke wa Sam Kutesa.

Sam Kutesa: Kwa wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Kutesa ni baba mkwe wa Muhoozi na shemeji kwa Rais Museveni.

Hope Nyakairu: Ni mpwa wa Janet Museveni ambaye ni anashughulikia masuala ya utawala na fedha Ikulu.

Meja Jenerali Jim Muhwezi: Ni shujaa wa vita vya msituni na mbunge wa Rujumbura ni shemeji kwa rais Museveni. Mke wa Muhwezi, Susan ni mpwa wa Janet Museveni. Muhwezi alikuwa akishughulikia fedha zinazotoka nje.

Susan Muhwezi: Ni mke wa Meja jenerali Muhwezi, yeye ni msaidizi wa Rais Musveni kwenye mpango wa ushirikiano wa biashara kati ya nchi za Afrika na Marekani (AGOA)

Chanzo: www.tanzaniaweb.live