Rais wa Uganda Yoweri Museveni amelaani shambulizi la Ijumaa Juni 16 huko Mpondwe, kusini-magharibi mwa Uganda, ambapo wanamgambo wanaohusishwa na Islamic State waliripotiwa kuwaua takriban watu 41.
“Ukatili huu mpya wa ADF ni uhalifu, ugaidi na ubatili,” alisema katika taarifa iliyoandikwa.
Wanafunzi 37 wa Shule ya Sekondari ya Mpondwe Lubiriha, mlinzi na watu watatu wa jamii jirani waliuawa katika shambulio la kuvizia usiku wa manane. Wanafunzi 6 wanaaminika kutekwa nyara huku wavamizi hao wakikimbilia Mashariki mwa D.R.C.
Bado haijabainika kwa nini shule hiyo, iliyokuwa ikijulikana kama Shule ya Sekondari ya Nyabugaando Peter Hunter ililengwa. Rais na Mkewe, Janet Museveni ambaye pia ni waziri wa Elimu wa nchi hiyo wamegusia ugomvi wa umiliki unaohusishwa na shule hiyo.
Hata hivyo, Dick Olum, Meja Jenerali wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda anayeongoza Kitengo cha Milimani anasema washambuliaji walilenga shabaha ndogo badala ya shule kubwa zaidi katika mji huo. Inaaminika kuwa watu 62 walikuwa shuleni wakati wa shambulio hilo.
UPDF ,Jumamosi, ilianzisha msako wa kuwasaka wavamizi hao, na kuahidi kupata matokeo ndani ya saa 24. Hata hivyo, hakuna hata mmoja wao aliyekamatwa au wanafunzi waliotekwa nyara kuokolewa.
Baadhi ya familia tayari zimeanza maandalizi ya maziko ya wafu.
Rais Museveni aliendelea kusema kuwa shambulio hili halitawazuia wanajeshi wa Uganda katika operesheni yao huko D.R.C.
“Sasa tunatuma wanajeshi zaidi katika eneo la Kusini mwa Mlima Rwenzori na kuondoa mapengo yoyote. King’ora kilipigwa na nani? Kwa nini watu wetu wa upande wa Kongo hawakuwa na ujasusi kuhusu kundi hili lililogawanyika,” alisema.
‘Tunaleta vikosi vipya upande wa Uganda tunapoendelea kuwinda upande wa Congo.” Rais Museveni amesema.