Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema mtandao wa kijamii wa ‘Facebook’ utafunguliwa tena nchini humo iwapo wataacha kutumika kuwashambulia.
Rais Museveni aliufungia mtandao wa Facebook kufanya kazi nchini kwake Januari 13, 2021, siku chache tu baada ya kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii kuondoa akaunti ghushi zilizohusishwa na Serikali yake kabla ya uchaguzi mkuu uliokuwa na ushindani mkali.
Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Daily Nation kilichomnukuu Rais Museveni wakati wa mazungumzo yake na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini humo yaliyofanyika juzi, alisema: “Facebook wana kiburi, walikuwa wakitumiwa kutushambulia, watu wetu walipojaribu kujibu walitufungia.
“Imepita miaka miwili tangu Facebook kukatazwa Uganda, nilipoangalia, bodaboda na teksi zilikuwa bado zinaendelea na shughuli zake pamoja na kukosekana kwa Facebook, natumai Facebook sasa inafahamu nani anaiongoza Uganda, watakapoacha kucheza michezo tutawafungulia”.
Matamshi hayo ya Rais yanakuja siku chache baada ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC), Irene Kagwa kusema Serikali inaisubiria Facebook kutatua changamoto zilizokuwepo kabla ya kufunguliwa tena kikamilifu.
“Kwa upande wetu, tunawangojea Facebook, tulizungumza nao na tukahitimisha. Kwa hiyo, masuala yaliyosalia yapo upande wao, kama Serikali tuko tayari kuirejesha mara tu watakapotimiza ahadi zao,” alisema.
Katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja kwenye runinga ya Taifa hilo, Museveni aliishutumu Facebook kwa kiburi na kusema “Hiyo chaneli ya kijamii unayozungumzia, ikiwa itafanya kazi Uganda inapaswa kutumiwa kwa usawa na kila mtu anayepaswa kuitumia,” alisema.