Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameanza kufanya mikutano na vigogo wa chama kinachotawala cha National resistance movement NRM kujua sababu zinazopelekea baadhi yao kupinga azma ya mtoto wake Generali Muhoozi Kainerugaba kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2026.
Kati ya wanaofanya vikao vya moja kwa moja na Museveni ni majenerali wastaafu ambao walipigana vita vilivyomuwezesha Museveni kuingia madarani mwaka 1986.
Museveni amefanya vikao na washirika wake wa karibu na wenye ushawishi ndani ya chama kinachotawala cha National resistance movement NRM na ambao wamesikika hadharani wakipinga kampeni ya Generali Muhoozi Kainerugaba kutaka kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2026.
Vigogo hao wa NRM wakiongozwa na Generali Mustaafu Kahinda Otafiire, wamekuwa wakisema kwamba watahakikisha kwamba Museveni anagombea mhula mwingine madarani, na kwamba hawawezi kumruhusu mwanawe, Generali Muhoozi kuongoza Uganda.
Muhoozi, ambaye alitangaza hivikaribuni kupitia ukurasa wake wa twiter kwamba atagombea urais, amejiita kuwa standby generator, yani mtambo mbadala wa kuzalisha umeme, wakati mfumo wa kawaida wa umeme unapozima, amekuwa akikosoa chama cha NRM akisema kwamba kimeoza na hakina tena uwezo wa kuongoza Uganda.
Lakini Vigogo wa chama wamekuwa wasikisitiza kwamba Muhoozi, hana sifa yoyote ya uongozi, saw ana generator iliyokufa. Wnataka Museveni kuendelea kuwa rais hazi atakapozidisha umri wa miaka 80.
Museveni, hajatangaza iwapo atagombea mhula mwingine lakini kila mara huwa anasema ni watu wake na chama chake ndio wanataka aendee kuwa rais.
Prof Mwambutsya Ndebeesaa ni mhadhiri wa siasa katika chuo kikuu cha Makerere, Uganda
“Anajaribu kumtengenezea mwanawe mazingira ya kisiasa ili itakapofika wakati wa uchaguzi mkuu, Muhoozi atakuwa amepata umaarufu kote nchini. Wanasaisa wengine hawaruhusiwi kufanya kampeni na wanapojaribu kufanya hivyo wanakabiliwa na nguvu kubwa za polisi. Sioni kama kuna mtu yeyote atasimama katika chama cha NRM na kupinga Muhoozi kuwa mgombea wa urais kwa sababu Museveni atawanyamazisha wote” amesema Prof Ndebesa.
Muhoozi ameanza kufanya kampeni
Museveni, anakutana na vigogo wa chama mmoja baada ya mwingine. Anataka kusikia kutoka kwo sababu zao za kukataa au kuidhinisha Generali Muhoozi kuwa mgombea wa urais.
Muhoozi anafanya kampeni kwa sasa licha ya kwamba ni mwanajeshi na sheria haimruhusu kufanya siasa.
Anasisitiza kwamba ansikiliza kilio cha raia wa Uganda ambao wanataka kuona mabadiliko, maana kwamba wanataka kuona babake akiondoka madarakani.
Muhoozi amekuwa akizuru nchini Rwanda mara kadhaa, mara ya mwisho ikiwa wiki hii, ambapo amedai kwamba amerejesha uhusiano mwema kati ya Rwanda na Uganda, hoja nayoitumia kama ujuzi wake wa kidiplomasia.
Wachambuzi wa saisa wanasema chama cha NRM kimepoteza ufuasi wa vijana na kuingiwa uoga, Generali Muhoozi akilenga kampeni ya mapema kumaliza nguvu za Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine.
Lakini baadhi ya raia wa Uganda kama Sadam Mubale, wana mtazamo kwamba umaarufu wa Muhoozi hauwezi kulinganishwa na umaarufu wa Bobi Wine
“Bobi Wine alikuwa na umaarufu hata kabla y kuingia katika siasa. Umaarufu wake upo kote nchini kutokana na muziki wake ulioangazia sana matatizo katika jamii na maswala ya kisiasa. Generali Muhoozi ameanza tu kujulikana kutokana na kupandishwa vyeo katika jeshi na watu kuanza kumzungumzia kwa kile kinaaminika kama anaandaliwa kuwa kumrithi babake.”
Kwa muda mrefu, wanasiasa, wanajeshi wa ngazi ya juu na wachambuzi wa siasa nchini Uganda wamekuwa wakidai kwmaba Museveni amekuwa akimtayarisha mwanawe, Generali Muhoozi Kainerugaba kumrithi.
Amepandisha cheo katika jeshi mara kadhaa kwa muda mfupi usivyokawaida katika jeshi, kiasi cha kufikia kiwango cha juu kabisa.
Kinachosubiriwa kutoka kwa Generali Muhoozi, ni kustaafu kutoka kwa jeshi na kugombea urais.