KATIKA kuhakikisha vita dhidi ya rushwa inakuwa endelevu, Rais Yoweri Museveni, amesema atapambana na kila mla rushwa, akianza na wenye tabia za aina hiyo katika ofisi yake.
Rais huyo ameonya kuwa, mfanyakazi yeyote wa Ikulu au yeyote katika utumishi wa umma atakayekutwa na hatia ya rushwa, ajiandae kwa kifungo gerezani.
Uamuzi huo wa Rais Museveni unashabihiana na ule unaochukuliwa wa marais wa nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk John Magufuli wa Tanzania, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Paul Kagame wa Rwanda, ambao wamekuwa mstari wa mbele kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya ofisi za umma.
Rais huyo wa Uganda alisema ofisi yake inapaswa kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya rushwa, hivyo hatarajii kuona kuna mtu anajihusisha na vitendo hivyo.
“Watumishi wa Ofisi ya Rais wanapaswa kuwa macho na masikio ya serikali katika kuona na kukemea vitendo vya rushwa. Lazima kila mmoja aepuke rushwa na kushiriki kikamilifu katika vita hii,” alisema.
Alisema watumishi wa idara ya usalama wa taifa katika ngazi zote, wanatakiwa kufichua vitendo vya rushwa na kuonya kwamba, kama kuna atakayepatikana akijihusisha badala ya kuzuia ataadhibiwa vikali.
Rais Museveni aliyewahi kuishi Tanzania, kupata elimu, kufanya kazi na hata kuanzisha familia, alisema atawatumbua viongozi wazembe katika vita dhidi ya rushwa.
“Wizi wa dawa katika vituo vya afya lazima ukomeshwe, mahali popote kutakakotokea vitendo vya rushwa maofisa wa usalama katika maeneo hayo watang’oka, hatutapenda kuona wakikumbatia rushwa na wizi wa mali za umma.”
“Kama watu wanateuliwa ili kumsaidia Rais wananchi wake lakini hawatimizi wajibu wao, kwa nini wasing’olewe na kuchukuliwa hatua zaidi? Lazima kila mmoja ashiriki kusafisha uozo wa rushwa,” alisema.
Rais Museveni aliwataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuaminiwa na kupandishwa vyeo, akijitolea mfano yeye mwenyewe kwamba alianza kazi Ikulu akiwa ofisa utafiti katika Ofisi ya Rais, lakini sasa ndiye anayeiongoza nchi.