Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakili TLS wapambana kusaka nafasi ya Fatma Karume

48471 PIC+MAWAKILI

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku 12 kabla ya Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kupata mrithi wa Fatma Karume, wagombea wa nafasi hiyo wameendelea kujinadi na ahadi za kuleta mageuzi makubwa ya uongozi 2019/2020.

Wagombea wa urais waliopitishwa na kamati ya uteuzi Machi 5, ni John Seka aliyeongoza chama hicho 2016/17, Charles Tumaini na Makamu wa Rais wa chama hicho, Dk Rugemeleza Nshala.

Wengine ni Godwin Ngwilimi aliyekuwa makamu wa Rais katika uongozi wa TLS Tundu Lissu na Godfrey Wasonga aliyejitokeza kwa mara ya pili mfululizo kugombea nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa TLS, wanachama 7,000 wanatarajiwa kupiga kura ya kuchagua jina moja kati ya hayo katika uchaguzi wa Aprili 6 jijini Arusha, siku moja baada ya kufunga kampeni.

Akizungumza jana, Dk Nshala alisema akipewa ridhaa, atasimamia utawala wa sheria za nchi, akisema baadhi ya viongozi wanatekeleza majukumu yao bila kuzingatia misingi ya utawala wa sheria.

“Pili, ninahitaji kuhakikisha mahakama zetu zinakuwa huru bila kuingiliwa na mawakili wanakuwa huru pia katika utekelezaji wa majukumu yao,” alisema.

Kuhusu kuhusishwa na siasa vyama, Dk Nshala alikana kuwa mwanachama wa chama chochote akisema anahudumia kila mteja bila kujali itikadi yake.

John Seka alisema endapo atakabidhiwa uongozi, ataimarisha uhusiano kati ya TLS na Serikali kupitia taasisi zake kama vile Jeshi la Polisi, Magereza na Mahakama ili kuimarisha demokrasia na haki za kila raia badala ya kuendelea kulumbana na taasisi hizo.

Kipaumbele cha pili kwa Seka kitakuwa ni kuunganisha wanachama vijana wanaoingia katika chama hicho, kuhakikisha wanajengewa uwezo na kufuata misingi ya haki wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kwa Watanzania.

“Eneo la tatu ni kushiriki kukuza demokrasia na masuala ya katiba, tutashirikiana na vyama vya siasa vyote katika kwa sababu ni majukumu ya TLS kisheria,” alisema Seka aliyekuwa rais wa TLS mwaka 2016/17, akimkabidhi Lissu kijiti.

Alipoulizwa sababu za kugombea kwa awamu nyingine, Seka alisema mwaka mmoja haukutosha kutekeleza malengo yake ndani ya chama hicho, hivyo anahitaji kuendeleza vipaumbele hivyo.

Wasonga akijinadi alitaja vipaumbele vinne ikiwamo kupunguza matumizi ya fedha za chama, kuhakikisha kila mwanachama anakuwa na bima ya afya, kuanzisha mradi wa ukumbi wa kibiashara Dodoma na kuongeza idadi ya wajumbe wa baraza la uongozi kutoka tisa hadi 18 ili kuwa na uwakilishi mzuri.

Kwa mujibu wa chama hicho kilichoanzishwa kwa Sheria ya Bunge ya 1954 Sura namba 307, mgombea wa urais anatakiwa kuwa mwanachama hai na aliyetumikia nafasi ya uwakili kwa zaidi ya miaka 10.



Chanzo: mwananchi.co.tz