Moto waliouwasha Mabingwa mara tatu mfululizo umewaka baada ya kubeba Mamilioni waliyoahidiwa kama wangeichapa Simba na Azam FC katika michuano ya Ngao ya Jamii.
Iko hivi, kabla ya mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii mabosi wa Yanga walikiita kikosi chao na kutoa ahadi kama wataifunga Simba watatoa 150 Milioni kama zawadi.
Na kama watavuka hatua hiyo na kushinda fainali basi kutakuwa na 150 Milioni zingine ambazo watazibeba.
Kazi ikaanza, katika nusu fainali ilikutana na Simba na kuwanyuka bao moja huku asisti ikitoka kwa Prince Dube na nyavu zikatikiswa na Max Nzengeli dakika ya 30 kipindi cha kwanza.
Baada ya hapo kibarua kikahamia Derby ya Mzizima ndani ya dakika 90 Miamba ikaweka mabao 4-1, wafungaji wakiwa ni Prince Dube,Clement Mzize na mawili walijifunga wao wenyewe Azam.
Kikosi hicho chini ya kocha Miguel Gamondi, kikawa kimemaliza hesabu za Mamilioni hayo kiulaini kabisa, huku kikitwaa Ngao ya Jamii ambayo msimu uliopita ilibebwa na Watani wao Simba.
Kama kawaida Waswahili wanasema ahadi ni deni, na mabosi ikabidi waitimize kwani kila walichokutana mastaa hao waliwapatia hivyo kazi ipo kwao tu.
Taarifa za ndani ya Simba zinasema Mohamed Dewji ‘Mo’ aliwaahidi kuwapa 300 Milioni kama wangetinga fainali lakini mambo yakawaendea tofauti.
Kumalizika kwa michuano hiyo kuna karibisha msimu kuanza, kwani dirisha la usajili litafungwa rasmi Agosti 15 na msimu utaanza Agosti 16.