Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Man United yakomaa na Mazraoui

Mazrouiiiii Man United yakomaa na Mazraoui

Fri, 26 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Manchester United itaongeza nguvu katika harakati za kusaka mabeki wa pembeni kutokana na wasiwasi uliozuka kwenye pande zote mbili za ulinzi nyuma.

Kikosi cha United cha watu 29 kiliondoka kwenda kwenye ziara ya pre-season huko Marekani juzi Jumatano bila ya Luke Shaw, Diogo Dalot na Tyrell Malacia. Aaron Wan-Bissaka, beki pekee ya timu ya wakubwa aliyepo ziarani, huenda akapigwa bei katika dirisha hili la uhamisho la majira ya kiangazi akihusishwa kutakiwa na West Ham na Galatasaray.

United itafikiria kusajili beki wa kushoto kutokana na wasiwasi wa Shaw kushindwa kudumu muda mrefu bila ya majeraha na hakuna dalili za Malacia kurejea mapema.

Hivyo, United imetoa macho sokoni kusaka beki mpya wa kulia katika dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi ili kuchukua nafasi ya Wan-Bissaka ambaye ameingia katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake.

Bissaka, 26, anaweza kuuzwa kwa Pauni 15 milioni, miaka mitano baada ya kuhamia Old Trafford akitokea Crystal Palace kwa ada ya uhamisho ya Pauni 50 milioni. United sasa inamtaka beki wa kulia wa Bayern Munich, Noussair Mazraoui.

Kwa ilivyo sasa, Dalot na Shaw watakuwa mabeki wa pembeni chaguo la kwanza. Dalot alikuwa mmoja wa wachezaji waliocheza kwa ubora msimu mzima uliopita baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano.

Hata hivyo, Shaw alicheza mechi 15 tu kutokana na majeraha ya misuli ya nyuma ya paja, na akapona katika muda mwafaka kuanzishwa katika mechi moja ya timu ya taifa ya England katika michuano ya Euro 2024.

Wachezaji wote waliopewa mapumziko baada ya fainali za Euro 2024 hawajajumuishwa katika kikosi cha United kilichoenda katika ziara ya mechi tatu huko Marekani.

Malacia, kwa upande wake, ameachwa Carrington aendelee kujiuguza baada ya kukosa msimu mzima uliopita kutokana na kufanyiwa upasuaji wa goti mara mbili.

Nafasi ya beki wa kushoto imekuwa tatizo kubwa United anapokosekana Shaw na Malacia – hasa baada ya Sergio Reguilon kurejea Tottenham mwisho wa mkataba wake wa mkopo Januari – huku Dalot, Wan-Bissaka, Victor Lindelof na kiungo Sofyan Amrabat wakichezeshwa katika eneo hilo.

Beki wa kati, Lisandro Martinez anaweza kucheza nafasi hiyo pia lakini Muargentina huyo alikosa sehemu kubwa ya msimu uliopita kutokana na majeraha ya kanyagio, goti na kiazi cha mguu.

Chanzo: Mwanaspoti