Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewajibu baadhi ya watu wanaokosoa ushauri wake kuwa sukari inayozalishwa Zanzibar kuuzwa kwanza kisiwani humo na ikiisha ndio iagizwe kutoka nje.
Majaliwa mbaye hivi karibuni alikuwa na ziara Zanzibar ameeleza hayo leo Alhamisi Januari 30, 2020 bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali hapo kwa papo.
Alikuwa akijibu swali la mbunge wa Baraza la Wawakilishi (BLW), Jaku Hashimu Ayoub aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itafikiria sukari inayozalishwa katika kiwanda cha Mahonda Zanzibar kuuzwa Tanzania Bara kama ilivyo kwa bidhaa nyingine zinazozalishwa Tanzania Bara na kuuzwa Zanzibar.
Katika majibu yake Majaliwa amesema katika ziara yake kisiwani humo, walikuta sukari nyingi kwenye kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha tani 24,000, “hivi sasa kinazalisha tani 6,000.”
“Mahitaji ya sukari Zanzibar ni tani 36,000 lakini nimeikuta bidhaa hiyo ghalani na mwekezaji analalamika hana soko. Nalazimika kuwa mkali kidogo, tumehamasisha wawekezaji kuja kuwekeza hapa na kuwahakikishia masoko lakini hatumpi masoko kwa sababu tunaruhusu sukari kuingia nchini wakati ya inayozalishwa ndani inabaki,” amesema Majaliwa.
Amesema licha ya kuwa Jaku anahitaji soko Tanzania Bara lakini mahitaji ya sukari Zanzibar ni tani 36,000 lakini sukari tani 6,000 hazina soko.
Pia Soma
- Mtazamo wa wananchi Maalim Seif kuutaka uwenyekiti ACT-Wazalendo
- Kangi Lugola, wenzake kuhojiwa Takukuru
- Wafanyabiashara Sao Hill kujibiwa Feb 17
Majaliwa amesema yeye na makamu wa pili wa Rais Zanzibar ndio wenye jukumu ya kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM na kwamba anaweza kwenda eneo lolote kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM.
“Ninapokuta ilani haitekelezeki lazima niwe mchungu lazima tuweke mpango wa kuwalinda wawekezaji wa ndani kuwahakikishia masoko na masoko tunayo,” amesema.
Ameongeza, “...,halafu mtu anasema nimewachefua Wazanzibar. Nimewachefua Wazanzibari ama nimewachefua wanunuzi?”
Amesema kuwa kiwanda hicho kinatoa ajira kwa watu 400, kinalipa kodi na kununua malighafi kutoka kwa wazalishaji wanaowazunguka.
Amesema wanaotamka kuwa wamechefuliwa ni wanunuzi na kwamba sera ni moja kuwalinda wawekezaji, wataendelea kuwa wakali pale wanapoona mambo hayaendi.