Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

London derby: Arsenal waanza kulialia

Capture Arsenal London derby: Arsenal waanza kulialia

Thu, 12 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Presha ipo juu. Ni kuhusu kipute cha North London derby baina ya Tottenham Hotspur na Arsenal kitakachopigwa wikiendi hii.

Kabla ya mechi, mashabiki wa Arsenal wameanza kulialia wakisema "msimu ufutwe" baada ya kumfahamu mwamuzi atakayechezesha mechi yao na mahasimu wao wakubwa kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta kitakwenda kwenye mechi hiyo kikiwakosa mastaa wake kibao baada ya sare ya bao 1-1 iliyopatikana kwenye mchezo wao uliopita dhidi ya Brighton.

Kiungo ghali kwenye kikosi hicho, Declan Rice alitolewa kwa kadi nyekundu katika mechi hiyo ya Brighton, hiyo ina maana hatakuwapo katika kipute cha Spurs. Kiungo mpya, Mikel Merino, naye atakuwa nje ya uwanja kwa miezi miwili baada ya kuumia bega mazoezini.

Nahodha wao, Martin Odegaard ni staa mwingine atakayekosekana baada ya kuumia enka wakati akiichezea Norway kwenye soka la kimataifa, pigo jingine ni la kuhusu beki Riccardo Calafiori, aliyeumia akiwa na timu ya taifa ya Italia.

Kutokana na hilo, kocha Arteta atalazimika kuanza na sura mpya katika kwenye kikosi chake cha kwanza na huenda Raheem Sterling akatumika kwa mara ya kwanza tangu aliponaswa kwa mkopo akitokea Chelsea kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi.

Hata hivyo, hilo wala haliwapi shida baadhi ya mashabiki wa Arsenal juu ya mchezaji gani atapangwa katika kipute hicho cha Spurs, Jumapili.

Lakini, wasiwasi wao upo kwa mwamuzi Jarred Gillett baada ya kuthibitishwa kwamba ndiye atakayechezesha kipute hicho cha London.

Mashabiki wa Arsenal wana historia na refa Gillett, ambaye alichezesha mechi yao ya kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Aston Villa msimu uliopita. John McGinn alifunga bao pekee katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba.

Lakini, mashabiki hao wa Arsenal wanaamini walimalizwa na mwamuzi Gillett kwenye mechi hiyo baada ya kushindwa kuwapa penalti kufuatia tukio la Douglas Luiz kumchezea rafu Gabriel Jesus akiwa ndani ya boksi la Aston Villa.

Na kwenye dakika za mwisho za mchezo huo, Kai Havertz aligomewa bao lake ambalo lilikuwa la kusawazisha uwanjani hapo Villa Park.

Mwamuzi Gillett alikataa bao hilo kwa madai kwamba mfungaji alikuwa ameunawa mpira. Marudio ya video ya tukio hilo yalionyesha Havertz na Cash wote mpira ulionekana kuwagusa mikono wakati walipokuwa wakigombea.

VAR iligoma kuingilia kati uamuzi wa mwamuzi huyo, hivyo msimamo ulibaki kwa Gillett kwamba halikuwa goli na Arsenal ikanyimwa fursa ya kukwepa kipigo katika mchezo huo uliokuwa wa upinzani mkali.

Arteta alionyesha hasira kali mechi ilipomalizika, alisema: "Ipo wazi kabisa ndio kawaida yao, ndio kawaida yao. Ninachomaanisha ndio hicho hicho. Hayo ndio maoni yangu, ndicho ninachoweza kusema.”

Na mashabiki wa Arsenal sasa wamevamia kwenye kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii kuonyesha wasiwasi wao mkubwa baada ya mwamuzi huo kuchaguliwa kuchezesha kipute hicho ambacho kwa namna fulani kitakuwa na maana kubwa kwenye mbio za ubingwa wa ligi.

Shabiki wa kwanza alisema: "Msimu ufutwe."

Mwingine aliongeza: "Naona kadi nyekundu kwa Gabriel na penalti kwa Spurs."

Na shabiki wa tatu alisema: "Hii tunataniana sasa."

Na shabiki wa nne aliongeza: "Nadhani tumeshamalizwa kwenye hiyo mechi ya Jumapili."

WAAMUZI WA KIPUTE

CHA SPURS vs ARSENAL

KWENYE EPL, SEPTEMBA 15

Mwamuzi wa kati: Jarred Gillett

Wasaidizi: Darren Cann, James Mainwaring

Mwamuzi wa akiba: Robert Jones

Mwamuzi wa VAR: Stuart Attwell

Msaidizi VAR: Constantine Hatzidakis.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live