Jumamosi ya Septemba 8, matajiri wa Chamazi, Azam FC walimtangaza, Rachid Taoussi kuwa kocha mkuu wa timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja akirithi mikoba ya Youssph Dabo aliyepewa mkono wa kwaheri.
Taoussi ambaye alitua nchini na wasaidizi wake watatu, kocha msaidizi, Ouajou Driss, kocha wa utimamu wa mwili, Badr Eddine na kocha wa makipa, Rachid El Mekkaoui, anakabiliwa na viunzi ambavyo vilimshinda aliyekuwa kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha.
Kama ambavyo ilikuwa kwa Benchikha, hii ni mara ya kwanza kwa kocha huyo mpya wa Azam kufanya kazi ukanda huu wa Afrika Mashariki huku rekodi za wawili hao zikionekana kufanana, sio aina ya makocha ambao wamekuwa wakikaa na timu kwa muda mrefu, hilo Azam wanatakiwa kujiandaa nalo.
Wakati Benchikha akitua Simba, Mwanaspoti iliripoti tabia za kocha huyo, licha ya kuwa na CV kubwa mara nyingi amekuwa mwepesi wa kubwaga manyanga ikiwa mambo yatakuwa ndivyo sivyo, ilikuwa hivyo miezi michache baadaye aling'atuka kwa sababu za kifamilia na kuibukia JS Kabylie.
Katika zaidi ya asilimia 80 ya timu ambazo Taoussi amezifundisha hakuna ambayo amedumu kwa zaidi ya misimu miwili, mfano mzuri wakati akiwa Raja Casablanca alifanya kazi kuanzia Machi mosi hadi Juni 23, 2022. Aliongoza timu katika michezo 15 tu na hicho ndio kilikuwa kibarua chake cha mwisho kabla ya kutua Bongo.
Hivi ndio viunzi ambayo kocha huyo anakabiliwa navyo.
UJENZI WA TIMU
Taoussi ameikuta Azam tayari imemaliza hesabu zao katika usajili, hivyo anakabiliwa na mtihani wa kukijenga kikosi hicho katika falsafa zake kulingana na wachezaji waliopo. Huu ni mtihani mgumu.
Mabosi wa Azam wanaamini kikosi chao ni bora na ndio maana walifanya uamuzi mgumu mwanzoni mwa msimu wa kumfuta kazi Dabo ambaye aliwafanya msimu uliopita kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa baada ya kumaliza ligi wakiwa nafasi ya pili, uwekezaji wao haukuendana na walichokiona.
Kati ya sifa za makocha kutoka Kaskazini mwa Afrika ni misimamo, kama ilivyokuwa kwa Benchikha pale Simba, Azam nao wanatakiwa kujiandaa kwa hilo maana Taoussi ni kocha muwazi na mwenye kusimamia kile ambacho amekuwa akikiamini, hivyo lolote linaweza kutokea.
Kwanini? Wakati akiwa FAR Rabat ya Morocco aliwahi kuwagomea mabosi wa timu hiyo na alikuwa tayari kuondoka walipotaka kumuingilia katika usajili, alihitaji aina ya wachezaji ambao alihisi wanaweza kuwa msaada kwake kulingana na malengo aliyowekewa.
PRESHA YA MATOKEO
Pamoja na jukumu mama na kukifanya kikosi hicho kuwa tishio mbele ya Simba na Yanga kwenye ligi kuwa sio kazi ya siku moja, kocha huyo atakuwa na mtihani wa kutafuta matokeo chanya ili asiwe kwenye presha.
Taoussi ambaye amekuwa akipenda kutumia mfumo wa 4-4-2 na 4-3-3 anatakiwa kutafuta namna nzuri ya kukabiliana na hili vinginevyo anaweza kuingia kwenye orodha ya makocha ambao walidumu Azam kwa kipindi kifupi zaidi.
Kocha wa zamani wa timu za vijana wa Azam FC, Mohammed Badru anaamini Taoussi anaweza kuwa na mafanikio huko Chamazi kutokana na uzoefu mkubwa alionao katika soka la Afrika pamoja na kwamba hii ni mara yake ya kwanza kufanya kazi ukanda huu wa Afrika Mashariki.
"Presha lazima awe nayo, hilo ni jambo la kawaida kwetu makocha, nadhani Azam imebarikiwa kwa kuwa na wachezaji wengi wenye ubora mkubwa, kilichopo na ambacho naona ni mtihani kwake ni juu ya namna ya kuwatumia wachezaji hao ili kupata kilichobora kutoka kwao.
"Mpira unahitaji ubora wa pamoja kama timu na sio mchezaji mmoja mmoja na kwa kuwa wachezaji wamekuwa pamoja kwa kipindi kirefu achana na maingizo mapya, wanaweza kufikia malengo, kikubwa ni kumpa ushirikiano," anasema kocha Badru.
UBORA WA WAPINZANI
Mwenzake Benchikha wakati akitua Simba aliikuta Yanga ikiwa bora, mazingira yale na haya ni sawa kwani bado timu ya Wananchi inaonekana kulishika soka la Tanzania maana wao ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho nchini hivyo Taoussi ana kibarua cha kuwazidi kete vijana hao wa Miguel Gamondi.
Matajiri wa Azam FC wakiongozwa na Yusuf Bakhresa wanatamani kuona timu yao ikiwa juu ya Simba na Yanga, hiyo ndio kiu yao kwa sasa na ndio maana wamemwaga mkwanja mrefu katika madirisha kadhaa yaliyopita ya usajili ili kuwa na wachezaji bora zaidi kwenye kikosi chao.
Azam tangu kuanzishwa kwake, imemudu mara moja tu kumaliza Ligi Kuu Bara ikiwa juu ya matani hao wa jadi na ilikuwa msimu wa 2013/14, ilifanya hivyo baada ya kukusanya pointi 62, Yanga ilishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 56, Simba ilikuwa ya nne ikiwa na pointi 38. Msimu huo Azam ilimaliza ligi bila ya kupoteza mchezo.
Azam ilicheza mechi nane za mwisho za msimu wa 2012-2013 na nyingine 26 za msimu mzima wa 2013-2014 ilipobeba taji lake pekee la ligi hiyo na nyingine nne za awali za msimu wa 2014-2015, na kuweka rekodi ya kucheza mechi 38 mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza. Rekodi hii ilikuja kuvunjwa na Yanga ilipocheza mechi 49 mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza.
WASIKIE AZAM
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabit Zakaria 'Zaka Zakazi' amesema, kitendo cha viongozi wa timu hiyo kumpa mkataba wa mwaka mmoja kocha huyo haina maana hawana imani naye, isipokuwa ni makubaliano ya pande mbili.
"Mkataba unasainiwa kwa makubaliano ya pande mbili, hatuwezi kufanya jambo kwa kumfurahisha kila mtu isipokuwa kwa kuzingatia malengo ya timu tuliyokubaliana kwa msimu mzima, hatuna shaka na uzoefu wake kwa alikopita," anasema Zaka Zakazi.