Dar es Salaam. Mahakama Kuu leo Jumatatu, Septemba 2, 2019, inaendelea na usikilizaji wa maombi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ya kibali cha kufungua shauri kupinga kukoma kwa ubunge wake.
Kiongozi wa jopo la mawakili wa Lissu, Peter Kibatala anaendelea kuwasilisha hoja za kuomba kibali katika hoja zake pamoja na mambo mengine amesema kuwa hatua zilizochukuliwa na Spika Job Ndugai kutangaza kuwa kiti cha Lissu kiko wazi kilifanyika bila haki ya upande wao kusikilizwa.
Kwa sasa Kibatala anaiomba Mahakama itoe amri kwa Spika kusimamisha kwa muda kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa CCM hadi mashauri hayo yatakapomalizika mahakamani.
Katika hoja zake Kibatala amewasilisha kesi mbalimbali za rejea zilizowahi kuamuliwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, kuhusu masuala anayoyaomba.
Awali Wakili Kibatala aliamua kuachana na ombi la Mahakama kumuamuru Spika ampatie Lissu taarifa ya kukoma kwa ubunge wake akidai kuwa tayari taarifa hiyo wameipata kupitia majibu ya wajibu maombi (Spika na AG) kwani zimeambatanishwa kama vielelezo kwenye hati zao za viapo kinzani.
Baada ya mawakili wa Lissu kumaliza kuwasilisha hoja zao, mawakili wa Serikali nao watasimama kujibu hoja hizo, kabla ya mawakili wa Lissu kusimama tena kujibu hoja mbalimbali zitakazoibuliwa na mawakili wa Serikali.
Habari zinazohusiana na hii
- Jinsi Jaji alivyoyatupilia mbali mapingamizi ya Serikali ya Tanzania dhidi ya Tundu Lissu
- Hoja iliyotikisa mahakamani maombi ya Tundu Lissu
Endelea kufuatilia kurasa zetu kwa taarifa zaidi