Timu ya GenGold imeendelea kufanya usajili ili kukiimarisha kikosi hicho kitakachocheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kutangaza wachezaji, Hija Ugando, Gerge Sangija na Helbert Lukindo kujiunga nao rasmi kwa msimu ujao.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imeeleza lengo la usajili huyo ni kuwapata baadhi ya wachezaji ambao wana uzoefu na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Sangija ambaye ni kiungo wa kukaba, alianza kuwika akiwa na Mbao FC, baadaye akasajiliwa na KMC, akatimkia Mbeya City na amesajiliwa na KenGold akiwa anatokea Geita Gold.
Lukindo ambaye ni straika, amesajiliwa kutoka Mbeya City, ambapo mbali na timu hiyo amezichezea Klabu za Mbao FC, Ndanda na Mgambo JKT.
Kwa upande wa Ugando ambaye naye ni straika, amesajiliwa kutoka Coastal Union, wasifu wake kisoka ukianzia kwenye kikosi cha pili cha Simba na kupandishwa timu ya wakubwa kuanzia mwaka 2015 na kucheza hadi 2017 alipohamia Coasta Union.
Usajili wa wachezaji hao unaifanya klabu hiyo ifikishe wachezaji watano ambao imewasajili kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.
Tayari imeshatangaza kumsajili mdogo wa winga wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, James Msuva, akitokea KMC, lakini ikipata saini ya straika hatari wa TMA Stars, Ramadhan Chobwedo, ambaye alikuwa mmoja wa waliofunga mabao mengi kwenye Ligi ya Championship msimu uliomalizika.
KenGold iilishinda vita ya kumwania straika huyo aliyekuwa akitakiwa kwa udi na uvumba na Prisons.
"Nimefurahi sana kwa kusajiliwa na KenGold, nipo hapa kuitetea nembo ya klabu hii, na ninawaahidi mashabiki wa timu kuwa tutapambana sana, japo ni wageni kwenye ligi, lakini lengo letu ikiwezekana ni kuchukua moja kati ya nafasi nne za juu, na ikishindikana kabisa basi tubaki kwenye ligi tukiwa kwenye nafasi nzuri," alisema Chobwedo.