Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli ya dalali sakata nyumba ya mtoto wa Mbowe kupigwa mnada

Mtoto Wa Mboweeeeeeeeeeeeeeee.jpeg Kauli ya dalali sakata nyumba ya mtoto wa Mbowe kupigwa mnada

Fri, 16 Feb 2024 Chanzo: mwanachidigital

Siku moja baada ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kuamuru kukamatwa na kupigwa mnada nyumba ya Mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe, dalali aliyekabidhiwa jukumu hilo amesema kuwa yuko tayari kuikamata muda wowote kuanzia sasa.

Nyumba hiyo iliyoamuriwa kukamatwa na kupigwa mnada, inayodaiwa kuwa ni ya Dadley ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, iko katika kiwanja namba 9, Mtaa wa Feza , Mikocheni B, barabara ya Chipaka.

Amri ya kukamatwa kwa nyumba hiyo ilitolewa jana Jumatano, Februari 14,2024 na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mary Mrio, ili kulipa deni la Sh62.7 milioni wanazomdai wanahabari walizokuwa wakifanya kazi kwenye gazeti hilo, baada ya mdaiwa huyo kushindwa kutekeleza makubaliano ya kuwalipa deni hilo ambalo ni malimbikizo ya mishahara yao.

Sambamba na amri hiyo, pia Mahakama ilimteua dalali wa kutekeleza amri hiyo, Jesca Massawe kutoka kampuni ya udalali ya MM Auctioneer & Debt Collectors.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo kufuatia maombi yaliyowasilishwa na wanahabari hao Maregesi Paul na wenzake 9 ili kutekeleza tuzo yao waliyopewa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), katika shauri la mgogoro wa kikazi waliloifungua dhidi ya mwajiri wao huyo.

Akizungumza jana Alhamisi, Februari 15, 2024, dalali huyo, amesema kuwa yuko tayari wakati wowote kuanzia kesho kukamata nyum,ba hiyo, baada ya kuelekezwa na wadai hao.

Massawe amesema kuwa baada ya kupata taarifa ya kutekeleza amri hiyo ya Mahakama, leo wamekwenda kuchukua hiyo amri mahakamani na walitarajia kuwa kesho wangeandaa notis na kumpelekea mdaiwa kisha kuikamata nyumba hiyo.

Amefafanua kuwa mali isiyohamishika mambo yote mawili yanaweza kufanyika kwa wakati mmoja, yaani kutoa taarifa kwa mdaiwa na kuikamata mali husika wakati huohuo.

Dalali huyo amefafanua zaidi kuwa ukamataji wa mali kama hiyo ni kubandika tu tangazo, na kuipiga picha kisha kupeleka taarifa na nyaraka ambatano katika ofisi ya Serikali ya Mtaa husika.

Hata hivyo amesema kuwa utekelezaji wa amri hiyo unaweza usikamilike kesho kutokana na tatizo la mawasiliano baina yake na wadai, akisema kuwa bado hajapata mawasiliano yao na wao hawajamtafuta.

“Sasa tatizo ni kwamba mimi sina mawasiliano yao sijayapata na nadhani na wao hawana mawasiliano yangu. Kwa hiyo wakishanitafuta tunaanza, hata ningekuwa nimepata mawasiliano yao leo, pengine tungeanza kesho huo mchakato."

Amesema kuwa kwa mpaka anazungumza jana muda wa saa 12:15 jioni wadai walikuwa hawajamtafuta na kwa kuwa kesho ni Ijumaa hiyo kazi hawezi kufanyika itasubiri mpaka Jumatatu.

Juhudi za kumpata mdaiwa huyo, Dadley hazikuzaa matunda kwani alipopigiwa simu mara kadhaa kupata maoni yake, muda wote ilikuwa ikiita tu bila kupokewa.

Wakati amri hiyo ilipotolewa jana Dudley hakuwepo mahakamani ingawa kwa mujibu wa wadai alikuwa ameahidi kuwepo pamoja na pesa za kuwalipa.

Awali wanahabari hao walifungua shauri hilo la mgogoro wa kikazi namba 28461 la mwaka 2023 CMA dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, baada mwajiri wao huyo kuvunja mitaba yao ya ajira.

Katika shauri hilo wadai walikuwa wakiomba kulipwa malimbizo ya mishahara yao jumla ya Sh114 milioni.

Hata hivyo CMA katika uamuzi wake uliotolewa na Mwenyekiti wa CMA, Bonasia Mollel Julai 17 mwaka 2023, iliamuru wadai walipwe Sh62.7 milioni, baada ya pande zote kukaa pamoja na kujadiliana na kufikia makubaliano ya pamoja.

Kwa mujibu wa Paul kufuatia makubaliano hayo Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30, 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa Februari mwishoni, 2024.

Hata hivyo hakutekeleza ahadi hiyo na baadaye wawakilishi wa wadai yaani Paul, Fidelis Felix, Arodia Peter na Exuperius Kachenje walikutana na Mbowe Desemba 20 na 21, 2023 nyumbani kwa wakurugenzi wa Gazeti hilo, Dudley na Lilian Mtei na kujadiliana kuhusu malipo hayo.

Katika majadiliano hayo inadaiwa kuwa Mbowe alikubali kulipa madai yao mwishoni mwa Desemba lakini naye hakufanya hivyo, ndipo wakawasilisha mahakamani maombi ya utekelezaji wa tuzo hiyo.

Katika maombi hayo waliomba mahakama itoe amri ya kukamata nyumba hiyo kwa kuwa mdaiwa amekaidi kutekeleza makubaliano ya kuwalipa, na mahakama ilikubaliana na hoja zao ndipo ikatoa amri hiyo na kumteua dalali huyo.

Mahakama iliahirisha shauri hilo mpaka Machi 4, 2024 litakapotajwa kwa ajili ya kupata taarifa ya utekelezaji wa amri hiyo.

Chanzo: mwanachidigital